Wanahisa wa Benki ya CRDB wameidhinisha gawio la shilingi 22 kwa hisa lililopendekezwa na Bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo katika Mkutano Mkuu wa 26 wa Wanahisa uliofanyika kidijitali siku ya jumamosi tarehe 22 Mei, 2021. Gawio ambalo ni ongezeko la asilimi 29.4 ya gawio liloidhinishwa mwaka jana, linatokana na matokeo mazuri ya kifedha ya benki hiyo katika mwaka wa fedha 2020 ambapo ilitangaza faida baada ya kodi ya Shilingi bilioni 165.2 licha ya changamoto zilizoletwa na COVID19.
Akiwasilisha taaarifa yake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay alielezea kuwa utendaji endelevu na mabadiliko ya kimkakati yanayoendelea ndani ya benki hiyo yamesaidia kufungua uwezo wa Benki, katika kuwahudumia wateja na kusaidia kuweka mazingira mazuri ya biashara. Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, utendaji wa Benki ya CRDB umeendelea kuimarika na kufanya uwekezaji wa wanahisa wake kuwa watija zaidi.
"Licha ya changamoto ambazo tulikutana nazo 2020, tulijidhatiti katika kuhakikisha wanahisa wetu wanapata faida kutokana na uwekezaji wao kama inavyojionyesha katika mapato kwa kila hisa. Tulipendekeza gawio la Shilingi 22 kwa kila hisa na ninafurahi kuwa julisha kuwa wanahisa wameliidhinisha, ”alisema Dk Laay.
Aliongeza: “jumla ya gawio lililopendekezwa ni Shilingi bilioni 58, ambalo linaashiria ukuaji wenye nguvu na maendeleo katika mapato kwa kila hisa na gawio kwa kila hisa. Ninapenda kuwajulisha kuwa Wanahisa wa Benki pia waliidhinisha Kampuni ya Ukaguzi wa Hesabu Ernst & Young kuwa Wakaguzi wetu wa nje wa mwaka fedha 2021, ikiashiria imani yetu katika utekelezwaji wao na kuendelea kwa Benki kufuata misingi ya utawala bora ”, alisema Dkt. Laay.
Dkt. Laay pia alibainisha kuwa katika kipindi cha mwaka jana, Benki ilipata mjumbe mpya wa Bodi, Bi. Ellen Gervas Rwijage, ambaye alijiunga na Bodi kama mwakilishi wa Mfuko wa Uwekezaji wa DANIDA (DIF), ambao una miliki hisa 21% ndani ya Benki.
Aliwaarifu pia Wanahisa kwamba Bi. Esther Kitoka, ambaye alikuwa Afisa Mkuu wa Uendeshaji aliondoka Benki na Bruce Mwile alichaguliwa kuziba nafasi hiyo. Kabla ya kuchaguliwa kwake, Bwana Mwile alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa tanzu ya Benki ya CRDB Burundi.
Wakati huo huo wanahisa wa Benki waliidhinisha mabadiliko ya katiba yaliyopendekezwa na Bodi ya Wakurugezi, na pia walipiga kura kuchagua wajumbe wawili wa bodi ambapo Prof Faustine Bee ilichaguliwa kwa mara ya pili kuwakilisha wanahisa wenye umiliki chini ya 1% na Gerald Kasatualichaguliwa kuwakilisha wanahisa wenye hisa kati ya 1% na 10%. Prof. Bee ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), wakati Gerald Kasatu ni Afisa Mkuu wa Uwekezaji katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF, Uganda.
Katika taarifa yake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alibainisha kuwa mapato ya Benki ya CRDB na kampuni zake yaliongezeka sana licha ya kushuka kwa uchumi kwa sababu ya Janga la COVID-19. Mapato ya uendeshaji yalisajili ukuaji wa asilimia 10.4 kufikia Shilingi bilioni 854 kulinganisha na Shilingi 774 zilizoripotiwa mwaka uliopita.
"Mkakati wetu wa kusaidia wateja wakati wa janga hilo kwa kiasi kikubwa ulitusaidia kuboresha mipango yetu ya biashara ili kuendana na mabadiliko," alisema Nsekela.
Nsekela pia alisema kuwa mabadiliko ambayo benki hiyo imekuwa ikiyafanya yameendelea kuleta matokeo chanya, huku akibainisha kuwa katika kipindi cha mwaka jana Benki ya CRDB iliwekeza kwa kiasi kikubwa katika mfiumo ya kidijitali. Uwekezaji huu ulipelekea kukua kwa idadi ya wateja wanaotumia njia za kidijitali, ambapo asilimia 87 ya miamala yote ilifanyika kidijitali.