Benki ya NMB imewapokea rasmi waliokuwa wafanyakazi wa Benki ya Biashara ya China (China Commercial Bank) ambayo umiliki wake ilikabidhiwa mwanzoni mwa mwezi huu na Benki Kuu ya Tanzania (BOT).
Wafanyakazi hao walipokelewa Makao Makuu ya NMB Jijini Dar es salaam na Uongozi na wafanyakazi wa benki hiyo. Akizungumza katika hafla ya mapokezi hayo Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB – Bi. Ruth Zaipuna alisema, ni Furaha kwao kama benki kuongeza ukubwa wa familia ya NMB na ametumia nafasi hiyo kuwakaribisha rasmi kuwa wanafamilia.
Bi. Zaipuna aliwahakikishia wafanyakazi hao kuwa wapo sehemu salama, kwani NMB ndio benki kubwa zaidi Tanzania kwa mtaji, mizania, faida, mtandao wa matawi na suluhishi za kibenki kwa wateja wao, huku wakiwa na matawi 226 nchini takribani katika wilaya zote, zaidi ya mawakala 8,000, zaidi ya mashine 700 za kutolea fedha (ATM) huku wakiwa na wateja zaidi ya milioni nne na wafanyakazi 3,400.
Bila kusahau kuwa NMB imekuwa ikishinda tuzo mbalimbali ikiwemo ya umahiri ya Euromoney kama “Benki Bora zaidi Tanzania” kwa miaka 8 mfululizo kuanzia mwaka 2013 hadi 2020. Benki hiyo pia ilipata tuzo ya Benki Salama zaidi Tanzania kutoka Jarida la Global Finance la nchini Marekani.
Naye Afisa Mkuu Rasilimali Watu wa NMB – Emmanuel Akonaay alisema, anategemea wafanyakazI hao wataendeleza yale yote mazuri waliyokuwa nayo na pia kuendelea kutoa huduma bora kwa waliokuwa wateja wao na wateja wengine wote wa Benki ya NMB.
Akizungumza kwa niaba ya wenzao - Phales Joseph Kiwanga, Aliishukuru Benki ya NMB kwa ujumla kwa ukaribisho na kuwa mwajiri wao mpya, huku akiahidi kufanya kazi kwa bidii na awadilifu mkubwa ili kuhakikisha NMB inabaki kuwa benki bora Tanzania.
No comments:
Post a Comment