Mkataba huo unaogharibu shilingi bilioni 3 za Kitanzania, umesainiwa baada ya ule wa awali uliosainiwa mwaka 2017, kufikia ukomu kati kati ya mwaka huu huku timu ikijivunia mafanikio mengi katika kipindi cha udhamini.
Akizungumza wakati wa utiaji saini wa mkataba huo mpya uliofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa SBL Mark Ocitti alisema kuwa, bia ya Serengeti Premium Lager ni mdau mkubwa wa michezo hapa nchini na kuongeza kuwa bia hiyo imekuwa ikijivunia kuwaunganisha Watanzania kupitia michezo.
“Kupitia bia yetu pendwa ya Serengeti Premium Lager, tunayo furaha kubwa kutangaza leo kutangaza udhamini kwa Timu yetu ya Taifa kwa kipindi kingine tena cha miaka mitatu. Tumechukua uamuzi huu kwa kuzingatia na kufahamu umuhimu wa michezo kwenye maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Tunaamini kwa kuidhamini Taifa Stars, siyo tu tunachangia katika maendeleo ya michezo bali pia tunachangia kukuza mpira wa miguu ambao watu wengi duniani na Tanzania wanaupenda sana,” alisema Mark
Mkurugenzi huyo aliongeza, “Tumeamua kusaini tena mkataba huu baada ya kuridhishwa na maendeleo pamoja na mafanikio ya timu kwa miaka mitatu iliyopita lakini pia kutoka na mapenzi makubwa ya Watanzania kwa timu yao ya taifa,”
Taifa Stars imefanikiwa kupata mafanikio makubwa chini ya udhamini uliomalizika wa bia ya Serengeti Premium Lager ikiwa ni pamoja na kuweza kufuzu na kucheza mashindano makubwa barani Afrika ya Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka jana ikiwa ni baada ya miaka 39 tangu kushiriki mara ya mwisho.
Udhamini huu mkubwa unakuja katika kipindi ambacho biashara nyingi katika ngazi ya kitaifa na kimataifa zinapunguza udhamini kwenye shughuli mbali mbali zikiwamo za kimichezo pamoja na kupuguza gharama za uendeshaji kutokana na janga la Corona ambalo limerudisha nyuma maendeleo ya biashara na mzunguko wa fedha duniani.
Akiishukuru bia ya Serengeti kwa udhamini huo, Rais wa TFF Wallace Karia alisema fedha zilizotolewa kwa ajili ya udhamini huo zitatumika kama ilivyokusudiwa na kuongeza kuwa zitasaidia sana katika kufanikisha uendeshaji ya timu na hivyo kupata matokeo mazuri katika michezo yake.
Kusainiwa kwa mkataba huu leo ni Ushahidi wa wazi kuwa bia ya Serengeti Lager ina imani ya kutosha na uongozi wa TFF na tunaahidi kuwa tutasimama imara kutumia udhamini huu kama mkataba unavyosema kwa manufaa ya timu yetu ya Taifa,” aliongeza Karia
Udhamini huu ni muendelezo wa bia ya Serengeti Premium Lager kuiunga mkono timu ya taifa, baada ya kufanya hivyo katika kipindi cha kati ya mwaka 2010 na 2012 na katika kipindi cha mkataba uliomalizika mwaka huu wa miaka mitatu na ambao ulisainiwa mwaka 2017.
No comments:
Post a Comment