Wafanyakazi wa kitengo cha Huduma kwa Wateja wakipozi kwa picha mara baada ya uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya Huduma kwa Wateja. |
Wiki hiyo inayoadhimishwa ulimwenguni kote imebeba kauli mbiu isemayo “Magic of Service” yaani huduma ya maajabu na imezinduliwa rasmi Oktoba 7 na itamalizika Oktoba 11.
Akizungumza wakati wa hafla iliyofanyika katika Kituo cha Huduma kwa Wateja cha Tigo, Meneja wa Huduma kwa Wateja, Mwangaza Matotola amesema wiki hii itaadhimishwa kwa aina yake kwa kuhimiza ubora wa huduma ili kuendana na mahitaji ya wateja.
“Huduma kwa wateja ni kitovu cha biashara yetu na ndiyo maana tunaweka kipaumbele katika kuhakikisha wateja wanapata huduma zenye ubora na weledi siku zote hivyo katika wiki hii tumejizatiti kuhimiza dhamira yetu ya kutoa huduma zenye kukidhi mahitaji ya wateja,” alisema Matotola.
Wiki hiyo itaambatana na matukio mbalimbali ikiwamo kutembelea kituo cha huduma kwa wateja, kujumuika na wateja pamoja na wadau ili kujadili namna bora zaidi ya kuendeleza huduma za kampuni hiyo.
Meneja huyo aliwahimiza wateja kutumia huduma mbalimbali za kimtandao kama WhatsApp, Twitter, Facebook na Instagram pale wanapohitaji huduma au msaada kutoka kwa wataalamu wenye weledi.
“Tigo imeendelea kuwekeza katika kuboresha huduma kwa kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wetu na zaidi tumewekeza zaidi katika kujenga miundombinu ya kituo chetu cha mawasiliano ili kuhakiisha wateja wanapata huduma za uhakika,” alisema
Aidha, wiki hiyo itahitimishwa kwa kutoa tuzo kwa mfanyakazi bora wa mwaka ambaye ameonesha weledi mkubwa katika utoaji wa huduma ikiwa ni njia ya kutoa hamasa kwa wafanyakazi wengine.
No comments:
Post a Comment