Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju (pichani juu) na Kaimu Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Bibi Lianne Houben (pichani chini) wakitoa hotuba fupi wakati wa Uzinduzi wa Mradi wa Kukua Na Kuku huko Kilacha, Moshi, Mkoani Kilimanjaro. Bofya hapa kwa picha zaidi |
Ubalozi wa Tanzania nchini Uholanzi kwa kushirikiana na Baraza la Biashara la Uholanzi na Africa (Netherlands – Africa Business Council - NABC) hivi karibuni waliongoza ujumbe wa Makampuni 7 kutoka Uholanzi yaliyobobea katika Sekta ya Ufugaji wa Kuku kwenda Mkoani Kilimanjaro kuzindua Mradi maalum wa ufugaji utakaoendeshwa na Makampuni hayo nchini Tanzania maarufu kama “Kukua Na Kuku (Growing with Chicken) Impact Cluster”.
Mradi wa “Kukua Na Kuku” ni matokeo ya makubaliano ya kuanzisha ubia kati ya Tanzania na Uholanzi yanayolenga kuboresha Sekta ya Ufugaji Kuku nchini Tanzania na kuifanya kuwa endelevu kwa kutumia teknolojia ya kisasa kutoka Uholanzi. Makampuni hayo yatatoa mafunzo kwa lengo la kuwajengea uwezo wafugaji wazawa kwa kuboresha usimamizi wa kilimo cha ufugaji, afya ya wanyama, upatikanaji wa chakula (lishe) bora kwa ajili ya mifugo, vifaa muhimu vya kufugia, na hata utafutaji masoko.
Uzinduzi huo ulifanyika kwenye Chuo cha Kilimo na Ufugaji wa Mifugo Kilacha, Mkoani Kilimanjaro kwa kusaini Makubaliano ya Ushirikiano, na ukawa ndio mwanzo wa ushirikiano wa miaka 3 kati ya makampuni hayo 7, Serikali ya Uholanzi na wadau wazawa wa Tanzania. Chuo cha Kilimo na Ufugaji wa Mifugo cha Kilacha kinasimamiwa na Kituo cha Uzalishaji na Mafunzo kinamilikiwa na Kanisa Katoliki Mkoani humo.
Mgeni rasmi wakati wa sherehe za uzinduzi huo alikuwa Mhe. Anna Mgwira, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro. Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju,Kaimu Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Bibi Lianne Houben, na Mkurugenzi wa Biashara na Kilimo wa NABC, Bw. Mackenzie Masaki.
Makampuni hayo kutoka Uholanzi ni pamoja na: Aeres University of Applied Sciences; Ebit+/I Grow Chicken; GD Animal Health; Impex; Hendrix Genetics; Koudijs de Heus; na Vencomatic Group.
|
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
No comments:
Post a Comment