Mbeya, 30 Julai, 2016: Benki ya TIB Corporate imetoa mchango wa shillingi milioni 10 kwa ajili ya kununua madawati ya wanafunzi wa shule za msingi za mkoa wa Mbeya ili kupunguza tatizo la uhaba wa madawati mkoani humo.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa benki ya TIB, Bw. Frank Nyabundege alisema ili wanafunzi waweze kufanya vizuri Katika masomo yao wanahitaji kuwa na mindombinu bora na mazingira mazuri ya kujifunza. 'Sisi kama taasisi tunaamini kuwa uhaba wa madawati ni tatizo kubwa sana katika maendeleo ya sekta ya elimu hivyo basi msaada huu utasaidia kupunguza tatizo hili katika sekta ya elimu nchini’ alisema Bw Nyabundege.
Bw.Nyabundege pia alieleza jinsi taasisi yake ilivyojizatiti katika kuhakikisha inashirikiana na serekali katika jitihada zake za kuboresha sekta ya elimu nchini.
'Mazingira rafiki ni muhimu sana kwa ajili ya kujifunzia,hivyo ni matumaini yetu mchango wetu wa madawati utachangia katika kuboresha zaidi mazingira ya wanafunzi na hivyo kuwahamasisha kuendelea kufanya vizuri katika masomo yao' alisema Bw. Nyabundege.
Akipokea msaada huo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw.Amos Makalla ameipongeza benki hiyo kwa kuwa mfano bora wa kushirikiana na serikali katika jitihada zake za kupunguza tatizo la uhaba wa madawati.
'Tunatoa shukurani zetu za dhati kwa benki ya TIB Corporate kwa mchango wao katika kuhamasisha na kusaidia kukua kwa kiwango bora cha elimu kwenye shule zetu’ alisema Bw. Makalla.
No comments:
Post a Comment