Dar es Salaam, Tanzania – Oktoba 5, 2026: Mteja anapokabidhi fedha zake, anaposhirikisha taarifa zake binafsi au anapopiga simu kuomba msaada, matarajio yake si kupata jibu la haraka pekee, bali pia kuhakikisha kuwa yuko salama.
Hili ni jambo ambalo Vodacom Tanzania imelipa kipaumbele katika Wiki ya Huduma kwa Wateja ya mwaka 2026, inayofanyika kuanzia Oktoba 5 hadi 9, kwa kuwapa wateja nafasi ya kufahamu kwa karibu hatua zinazochukuliwa kuwalinda wao, fedha zao na taarifa zao binafsi, pamoja na mambo wanayoweza kufanya ili kujilinda dhidi ya udanganyifu.
Takwimu zinaonesha kwa nini suala hili ni muhimu. Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hadi Juni 2026 kulikuwa na akaunti milioni 87 za huduma za fedha kwa njia ya simu nchini. Katika kipindi hicho, TCRA ilirekodi jumla ya majaribio 7,334 ya udanganyifu.
Ingawa idadi hiyo ilipungua kwa asilimia 25.29 ikilinganishwa na robo iliyotangulia, bado inaonesha kuwa udanganyifu ni changamoto inayohitaji watumiaji wa huduma za simu kuwa makini.
![]() |
| Brigita Shirima (kushoto), Mkurugenzi wa Biashara na Masoko wa Vodacom Tanzania PLC, akimkabidhi zawadi mteja wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja jijini Dar es Salaam, Oktoba 5, 2026. |
Kwa Vodacom Tanzania, usalama wa mteja unaanzia kwenye kuhakikisha kuwa mtu sahihi ndiye anayepata huduma kwenye akaunti husika. Usajili wa laini za simu unahusisha uthibitishaji wa alama za vidole dhidi ya taarifa za NIDA, na utaratibu huo hutumika pia wakati wa kubadilisha laini za simu.
Mabadiliko ya laini za simu hayawezi kufanyika kwa niaba ya mtu mwingine, hatua inayolenga kuimarisha usalama wa wateja na kuzuia matumizi yasiyoidhinishwa ya akaunti zao.
“Wateja wetu wanatuamini na kutukabidhi sehemu muhimu za maisha yao ya kila siku, ikiwemo fedha zao na taarifa zao binafsi. Imani hiyo inakuja na wajibu wa kuhakikisha wateja wetu wako salama. Wiki ya Huduma kwa Wateja inatupa nafasi ya kuwaonesha hatua tunazochukua kuwalinda, lakini pia kuwakumbusha kuwa nao wana nafasi kubwa katika kujilinda,” alisema Mkurugenzi wa Kitengo cha Shughuli za Huduma kwa Wateja wa Vodacom Tanzania PLC, Harriet Lwakatare.
Utaratibu huo unaendelea pia pale mteja anapowasiliana na Huduma kwa Wateja. Kabla ya kusaidiwa, mteja huthibitishwa kuwa ndiye mmiliki wa akaunti.
Wakati huohuo, Vodacom inaendelea kuwakumbusha wateja jambo muhimu kuhusu usalama wa fedha zao: kamwe usimpe mtu yeyote namba yako ya siri ya M-PESA, hata kama anajitambulisha kuwa ni mfanyakazi wa Vodacom.
Na pale mteja anapohisi kuwa kuna jambo haliko sawa, kutoa taarifa mapema kunaweza kusaidia.
Timu ya Vodacom Tanzania inayoshughulikia masuala ya udanganyifu hushirikiana na wateja kufuatilia namba za simu au barua pepe zinazohusishwa na tukio lililoripotiwa. Pale inapohitajika, timu hiyo pia hushirikiana na Jeshi la Polisi katika uchunguzi na hatua za kisheria.
Kwa sababu hiyo, wateja wanahimizwa kutoa taarifa haraka wanapohisi wamekutana na tukio la udanganyifu, badala ya kusubiri.
Hatua za kupata msaada pia zimerahisishwa. Wateja wanaweza kuwasiliana na Huduma kwa Wateja ya Vodacom kwa kupiga 100 au 101, kutuma ujumbe kupitia WhatsApp kwa +255 754 100 100, kutuma barua pepe kupitia customercare@vodacom.co.tz, au kufika katika duka la Vodacom au dawati la Huduma kwa Wateja.
Kwa wateja wanaopendelea kujihudumia wenyewe, App ya My Vodacom inawawezesha kupata huduma mbalimbali bila kutumia data. Wateja pia wanaweza kutumia huduma ya kufungua PIN ya M-PESA kila siku.
Vodacom Tanzania inawahimiza wateja kufanya usalama kuwa sehemu ya matumizi yao ya kila siku ya simu kwa kutumia njia rasmi za Vodacom, kuhakikisha wanajua wanayewasiliana naye kabla ya kutoa taarifa au kutuma fedha, na kuripoti mara moja jambo lolote la kutiliwa shaka kupitia Huduma kwa Wateja kwa namba 100.
Wateja pia wanaweza kuangalia namba za simu zilizosajiliwa kwa kutumia kitambulisho chao cha NIDA, hatua inayowasaidia kufahamu namba zote zinazohusishwa na utambulisho wao.
Wiki ya Huduma kwa Wateja huadhimishwa duniani kote katika wiki ya kwanza kamili ya mwezi Oktoba. Katika maadhimisho ya mwaka huu, Vodacom Tanzania itaendelea kutumia vyombo vya habari na mitandao yake ya kijamii kuwafikishia wateja taarifa muhimu kuhusu usalama, namna ya kupata msaada na hatua wanazoweza kuchukua ili kujilinda.
Kwa sababu huduma nzuri kwa mteja si kuwa tayari kusaidia tu pale tatizo linapotokea. Ni pia kumsaidia mteja kujua namna ya kujilinda kabla tatizo halijatokea.
Fuata Kitomari Banking & Finance Blog kwa habari na uchambuzi kuhusu biashara, benki, fedha, teknolojia ya kifedha na sekta mbalimbali za uchumi.




No comments:
Post a Comment