Foreign Exchange Rates

CRDB Bank Advert_070325

Selcom Pesa Advert_110225

Selcom Pesa Advert_110225

Standard Chartered Advert_300125

Standard Chartered Advert_300125

Monday, 1 September 2025

NMB YAAHIDI USHIRIKIANO MKUBWA ZAIDI KUKUZA SEKTA YA UTALII NCHINI

Arusha – Benki ya NMB imewahakikishia wafanyabiashara wakubwa wa mkoa wa Arusha ushirikiano wa karibu zaidi katika kukuza shughuli zao, hususan sekta ya utalii, ili kuongeza ufanisi wa kibiashara, mapato, na mchango wa taifa katika uchumi wa dunia.

Akizungumza katika hafla ya chakula cha jioni iliyowakutanisha zaidi ya wafanyabiashara 100 wakubwa wa mkoa huo, Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Ruth Zaipuna, alisema benki hiyo inatambua mchango mkubwa wa Arusha katika sekta ya utalii na biashara kwa ujumla, hivyo itaendelea kushirikiana nao kuhakikisha sekta hiyo inazidi kustawi.

“Moja ya jukumu letu ni kuhakikisha ustawi na uendelevu wa biashara zenu. NMB imekuwa ikibuni bidhaa na huduma za kifedha zinazolenga kuondoa changamoto mnazokutana nazo, kuanzia mikopo yenye riba nafuu, teknolojia bunifu za kidijitali, hadi mifumo rahisi ya malipo,” alisema Zaipuna.

Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), sekta ya utalii imeendelea kuwa kinara katika kuingiza fedha za kigeni nchini, ambapo imefanikiwa kuvutia watalii milioni 5.3 na kuingiza zaidi ya dola za Marekani bilioni 4, hatua iliyoiweka Tanzania miongoni mwa vinara wa utalii barani Afrika.

Zaipuna alisisitiza kuwa mchango wa sekta binafsi, hususan wafanyabiashara wa Arusha, ni nyenzo muhimu kufanikisha mafanikio hayo. Pia aliwataka wafanyabiashara kuendelea kutoa mrejesho wa huduma na mapendekezo ya bidhaa mpya ili benki iweze kubuni suluhu zinazokidhi mahitaji yao.

Kwa upande wake, Ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, alisema benki hiyo yenye thamani ya mali (assets) zaidi ya shilingi trilioni 4, ina uwezo wa kumkopesha mteja mmoja hadi shilingi bilioni 600.

“Hii ni ishara kuwa tumejidhatiti kikamilifu kutoa masuluhisho ya kifedha, kuanzia mikopo ya uwekezaji, malipo ya kidijitali, huduma za bima na ushauri wa kifedha,” alisema Mponzi.

Aliongeza kuwa uimara huo umeifanya NMB kutambuliwa kama benki salama zaidi nchini kwa miaka mitatu mfululizo, sambamba na kushinda mara 11 tuzo ya Benki Bora Tanzania kutoka jarida la kifedha la Euromoney katika kipindi cha miaka 13 iliyopita.

Huduma Maalum kwa Sekta ya Utalii

Mponzi alieleza kuwa NMB inatoa mikopo kwa ajili ya kuendeleza biashara za malazi ya wageni, ujenzi wa kambi na mahema ya kifahari (luxury tents), ununuzi wa magari ya usafiri wa watalii, pamoja na mikopo ya kulipia vifaa kwa awamu kwa riba nafuu.

Mmoja wa wafanyabiashara waliohudhuria, Frank Kileo, aliipongeza NMB kwa ukaribu wake na wadau wa biashara:

“Tunaona benki yenu imeendelea kuwa kinara licha ya ushindani mkubwa sokoni. Hili linatupa imani kama wateja na kutufanya tujione tuko salama zaidi. Endeleeni kujiimarisha kukabiliana na ushindani uliopo,”alisema.

Naye Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa NMB, Baraka Ladislaus, alisema lengo la hafla hiyo lilikuwa ni kusikiliza changamoto za wafanyabiashara, kupata mrejesho wa huduma, na kutoa elimu kuhusu bidhaa mpya ikiwemo teknolojia za malipo, kadi bunifu, pamoja na bima za usafiri, afya, mizigo na safari.





No comments:

Post a Comment