Dar es Salaam, Agosti 2025 – Katika hatua ya kihistoria ya kuimarisha dhamira yake ya kuwapa wateja huduma bora, Exim Bank imezindua rasmi huduma yake ya ‘Elite Banking’, ikiwa ni mwendelezo wa uvumbuzi unaolenga kuboresha uzoefu wa wateja katika sekta ya fedha.
Uzinduzi huo ulifanyika katika hafla ya kifahari iliyowakutanisha wateja mashuhuri, wajumbe wa bodi ya wakurugenzi, na washirika wa benki hiyo katika Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.
Huduma ya Kipekee Kwa Mahitaji ya Kisasa
Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Exim Bank Tanzania, Bw. Jaffari Matundu, alitoa shukrani kwa wateja wao waliowekwa mbele kama nguzo ya mafanikio ya benki hiyo.
“Elite Banking si huduma mpya tu, bali ni ishara ya dhamira yetu ya kuwaweka wateja wa thamani katika kila tunachokifanya,” alisema Bw. Matundu.
Alisema kuwa lengo kuu la huduma hii ni “Kutafsiri Upya Dhana ya Upekee”, kutoka kwenye mtazamo wa jadi wa hadhi kwenda kwenye huduma za kibinafsi, zinazotambua na kutanguliza mahitaji halisi ya wateja.
“Upekee huu mpya unahusu zaidi ya bidhaa za kifedha. Unaakisi dhamira yetu ya kutoa uzoefu wa kibinafsi, huduma maalum, na ufumbuzi unaozidi matarajio ya mteja,” aliongeza.
Huduma za Kidigitali na Timu Maalum ya Mahusiano
Kwa upande wake, Andrew Lyimo, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Rejareja Exim Bank, alifafanua kuwa huduma ya Elite Banking imeundwa mahsusi kwa ajili ya wateja wa hadhi ya juu kwa kuzingatia urahisi, teknolojia, na huduma binafsi.
“Huduma hii inawapa wateja wetu upatikanaji wa huduma za kifedha popote walipo, kupitia maeneo maalum ya kusubiria katika matawi, huduma za kimataifa viwanja vya ndege kupitia Mastercard DragonPass, pamoja na suluhisho bunifu za kifedha zilizoboreshwa kwa hadhi yao,” alisema.
Huduma hii ni muendelezo wa mafanikio ya mpango wa Preferred Banking ulioanzishwa mwaka 2016, na sasa imepanuliwa zaidi kwa huduma za haraka, za kipekee na zenye ubora wa hali ya juu.
Uzinduzi wa Kadi za Mastercard World
Kilele cha hafla hiyo kilikuwa ni uzinduzi rasmi wa kadi tatu za kifahari za Mastercard World, ambazo ni:
- Mastercard World Debit Card (TZS)
- Mastercard World Debit Card (USD)
- Mastercard World Credit Card
Kadi hizi zimeundwa kwa kushirikiana na kampuni ya Mastercard, na zinawapa wateja wa Elite Banking fursa ya kupata huduma bora zaidi kama vile maeneo maalum ya kusubiria kwenye viwanja vya ndege duniani kote, usafiri wa kifahari, bima ya kina ya usafiri (ajali, matibabu ya dharura), na ulinzi wa manunuzi duniani kote. Pia, wateja watanufaika na zawadi za kipekee kupitia milo, burudani, usafiri na manunuzi—yote yakiongozwa na teknolojia ya kisasa ya malipo isiyo ya kutumia fedha taslimu (cashless).
Ushirikiano na Mastercard
Elsie Wachira-Kaguru, mwakilishi wa Mastercard kwa Tanzania, Burundi na Djibouti, alielezea furaha ya kampuni yao kushirikiana na Exim Bank katika uzinduzi huu.
“Mastercard tunajivunia kuendeleza mapinduzi ya malipo ya kidijitali nchini Tanzania. Huduma hii mpya ni ishara ya dhamira yetu ya kuwapa wateja fursa zisizo na mipaka kupitia ushirikiano wenye manufaa kama huu,” alisema.
Kuelekea Upekee Wenye Maana
Kupitia huduma ya Elite Banking, Exim Bank Tanzania inafungua ukurasa mpya wa huduma za kifedha zinazokidhi mahitaji ya karne ya 21, huku ikibadilisha tafsiri ya upekee kuwa huduma za kweli zenye mshiko — zinazojengwa juu ya uaminifu, teknolojia, na uwezeshaji wa wateja kufikia malengo yao makubwa.
Kuhusu Exim Bank Tanzania
Exim Bank Tanzania ni miongoni mwa taasisi kubwa za kifedha nchini, inayotambulika kwa huduma bora, uvumbuzi unaomlenga mteja, na upanuzi wake wa huduma hadi nje ya mipaka ya Tanzania. Benki inaendelea kuweka viwango vipya katika huduma za kibenki za kisasa.
Kuhusu Mastercard
Mastercard ni kampuni ya teknolojia ya kimataifa katika sekta ya malipo, yenye dira ya kuunganisha na kuwezesha uchumi jumuishi wa kidijitali unaowanufaisha wote – kila mahali. Kampuni hiyo inalenga kuhakikisha miamala ni salama, rahisi, ya haraka, na yenye upatikanaji mpana kwa wote.
No comments:
Post a Comment