DAR ES SALAAM, Agosti 1, 2025: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametembelea tawi jipya la Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) lililopo Ubungo, Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi rasmi wa Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC).
Tawi hilo jipya la NBC limejengwa ndani ya jengo la kisasa la EACLC ambalo ujenzi wake ulianza mwezi Mei 2023 na kugharimu Shilingi bilioni 282.7 hadi kukamilika kwake. NBC ni miongoni mwa taasisi za kifedha zilizofadhili ujenzi huo, ikiwa ni sehemu ya dhamira yake ya kuchochea biashara, usafirishaji, ajira, na maendeleo ya kiuchumi nchini.
RAIS SAMIA AVUTIWA NA HUDUMA ZA KISASA ZA NBC
Rais Samia, akiwa ameambatana na viongozi waandamizi wa serikali akiwemo Waziri wa Nchi – Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo, alitembelea tawi hilo jipya ambapo alipokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Bw. Theobald Sabi, pamoja na maofisa waandamizi wa benki hiyo.
Akizungumza mbele ya Rais, Bw. Sabi alimpongeza Rais Samia kwa uongozi wake imara unaoweka mazingira bora ya uwekezaji nchini. Alisema uanzishwaji wa tawi hilo ni sehemu ya jitihada za NBC kuunga mkono malengo ya serikali kwa kutoa huduma bora na za kisasa za kifedha, hasa kwa wafanyabiashara wa ndani na wa kimataifa.
TAWI LA KISASA LENYE HUDUMA KAMILI ZA KIFEDHA
“Tawi hili ni ‘fully-fledged’, linatoa huduma zote za kibenki zikiwemo mikopo na ATM za kisasa zinazowezesha kutoa fedha za Kitanzania na za kigeni (Multi-currency),” alisema Bw. Sabi. Aliongeza kuwa tawi hilo litakuwa likitoa huduma hadi saa 1:00 usiku — sawa na tawi la Mlimani City — ili kuendana na mahitaji ya biashara za kimataifa na ratiba za wafanyabiashara.
Pia alieleza kuwa benki hiyo imedhamiria kurahisisha malipo ya serikali kutoka kwa wafanyabiashara waliopo katika kituo hicho, hatua itakayohakikisha mamlaka za serikali zinapata makusanyo kwa wakati na kwa urahisi.
NBC YADHAMIRIA KUSUKUMA MBELE MAENDELEO YA TAIFA
“NBC ipo tayari kuwa mshirika wa kweli wa serikali na sekta binafsi katika kukuza biashara, kuwezesha wajasiriamali, na kuendeleza ajenda ya maendeleo ya taifa letu,” alisisitiza Bw. Sabi.
Kwa sasa, uzinduzi wa tawi hilo la Ubungo unaifanya NBC kufikisha jumla ya matawi 22 jijini Dar es Salaam, sambamba na zaidi ya mawakala 7,200 wa NBC Wakala. Hii ni hatua muhimu katika kuimarisha ujumuishaji wa kifedha na kuwawezesha wananchi wengi zaidi kushiriki katika sekta rasmi ya fedha.
Usikose kufuatilia Kitomari Banking & Finance Blog kwa habari zaidi kuhusu maendeleo ya sekta ya fedha, benki, na biashara nchini Tanzania.






No comments:
Post a Comment