Foreign Exchange Rates

CRDB Bank Advert_070325

Selcom Pesa Advert_110225

Selcom Pesa Advert_110225

Standard Chartered Advert_300125

Standard Chartered Advert_300125

Sunday, 3 August 2025

BALOZI WA UINGEREZA AZURU KIWANDA CHA SBL MOSHI, AKISIFIA MCHANGO WAKE KATIKA UCHUMI WA TANZANIA

Kilimanjaro, Tanzania, 1 Agosti 2025 – Kufuatia ziara yake yenye mafanikio jijini Dar es Salaam mwezi Juni mwaka huu, Mhe. Marianne Young, Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, ameendelea na ziara yake kwa kutembelea kiwanda cha bia cha Serengeti Breweries Limited (SBL) kilichopo Moshi.

Ziara hii imeonesha kwa uwazi uhusiano wa karibu wa kiuchumi kati ya Uingereza na Tanzania, huku ikisisitiza mchango mkubwa wa SBL katika kutoa ajira kwa Watanzania, kuwezesha wakulima, kukuza kilimo, na kuchangia mapato ya serikali.

Uwepo wa Balozi huyo mkoani Kilimanjaro unaonesha upana wa shughuli za SBL nchini, na namna kampuni hiyo inavyotoa mchango wa moja kwa moja katika kukuza uchumi wa mikoa na kuleta fursa za maendeleo kwa jamii mbalimbali. Ziara hiyo imekuwa pia fursa ya kujifunza kwa undani kuhusu dhamira ya SBL ya kutumia mazao ya ndani na kuwekeza katika ustawi wa jamii zinazozunguka maeneo ya viwanda vyake.

“Ni heshima kubwa kwetu sisi kama SBL kumpokea Mhe. Balozi Marianne Young hapa katika kiwanda chetu cha Moshi leo. Ziara hii ni uthibitisho wa ushirikiano thabiti kati ya Uingereza na Tanzania, na pia inatupa fursa ya kuonesha matokeo ya moja kwa moja ya uwekezaji wetu. Hatujazalisha vinywaji tu, bali tunakuza maisha,”
alisema John Wanyancha, Mkurugenzi wa Mahusiano kwa Umma wa SBL.

Aliongeza kuwa dhamira ya kampuni hiyo ni kuwawezesha zaidi ya wakulima 600 wa ndani kupitia programu za ununuzi wa mtama, mahindi na shayiri, zikiwemo mpango wa Shamba ni Mali na Kilimo Viwanda, ambazo hutoa mafunzo ya kilimo bora, mbegu zenye ubora wa hali ya juu, na soko la uhakika – hatua zinazochangia kuongeza kipato na kuinua maisha ya wakulima hao.

“Shughuli zetu hapa Moshi, Mwanza na Dar es Salaam zimekuwa chanzo kikuu cha ajira rasmi na zisizo rasmi kwa maelfu ya watu, huku mchango wetu mkubwa wa kodi ukiwa ni nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa,” aliongeza Wanyancha.

Katika ziara hiyo, ujumbe wa Balozi ulipata maelezo ya kina kuhusu mchakato wa uzalishaji wa bia, udhibiti wa ubora, pamoja na mikakati ya baadaye ya kampuni ambayo kwa kiwango kikubwa yanategemea mazao ya kilimo ya ndani. Aidha, walifahamishwa namna SBL inavyotoa mchango wa kiuchumi, ikiwemo kulipa kodi inayosaidia serikali kufanikisha utoaji wa huduma za jamii na maendeleo ya miundombinu.

Kwa upande wake, Mhe. Young alisema:

“Ni jambo la kuvutia sana kushuhudia kwa macho yangu ukubwa na faida za shughuli za Kampuni ya Bia ya Serengeti hapa Moshi. SBL ni mfano bora wa jinsi uwekezaji wa kigeni unaowajibika – hasa kupitia kampuni inayomilikiwa na Diageo – unavyoweza kuchochea maendeleo shirikishi ya kiuchumi.
Kuanzia utoaji wa ajira kwa maelfu ya Watanzania, kuwawezesha wakulima, hadi mchango wao mkubwa wa mapato kwa serikali, ni wazi kuwa SBL ni mdau muhimu katika mafanikio ya kiuchumi ya Tanzania. Uingereza inajivunia kuunga mkono kampuni zinazochochea maendeleo endelevu na kushirikiana kwa dhati na jamii za ndani, hususan katika sekta ya kilimo.”

Ziara hii inaonesha maono ya pamoja kati ya Uingereza na Tanzania ya kujenga uchumi imara na jumuishi, unaojengwa juu ya misingi ya maendeleo endelevu na ushirikiano wa karibu kati ya sekta binafsi na ya umma.

SBL inaendelea kuwa mfano wa biashara inayowajibika kwa jamii, ikithibitisha kwamba mafanikio ya kibiashara yanaweza kwenda sambamba na maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.


KUHUSU SBL

Ilianzishwa mwaka 1988 kama Associated Breweries, Serengeti Breweries Limited (SBL) ni kampuni ya pili kwa ukubwa wa uzalishaji wa bia nchini Tanzania, ikiwa na zaidi ya asilimia 25 ya hisa ya soko.

SBL ina viwanda vitatu vya uzalishaji vilivyopo Dar es Salaam, Mwanza na Moshi. Tangu mwaka 2002, kampuni imeendelea kuongeza chapa zake kila mwaka, huku ununuzi wa hisa nyingi na EABL/Diageo mwaka 2010 ukichangia kuongezeka kwa uwekezaji, viwango vya kimataifa vya ubora, na nafasi nyingi zaidi za ajira kwa Watanzania.

Chapa zake maarufu ni pamoja na:

  • Serengeti Premium Lager
  • Serengeti Lite
  • Serengeti Lemon
  • Pilsner Lager
  • Kibo Gold
  • Guinness Stout
  • Guinness Smooth
  • Senator

Kampuni hii pia inazalisha vileo vya kimataifa vinavyotambuliwa duniani kama vile Johnnie Walker Whisky, Tequila, Smirnoff Vodka, Gordon’s Gin, Captain Morgan Rum na Baileys Irish Cream.


KWA TAARIFA ZAIDI, WASILIANA NA:

Rispa Hatibu
Meneja Mawasiliano na Uendelevu – SBL
📞 Simu: +255 685 260 901
📧 Barua pepe: Rispa.Hatibu@diageo.com



No comments:

Post a Comment