Dar es Salaam, Julai 23, 2025 — Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania na kampuni ya Sunderland, wamezindua rasmi mfumo wa kisasa wa mauzo ya jezi za timu ya taifa, Taifa Stars, kwa njia ya mtandao. Hatua hii inalenga kurahisisha upatikanaji wa jezi hizo kwa wananchi wote hususan kuelekea mashindano ya CHAN 2025.
Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam, ukiongozwa na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma (Mwana FA), na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo wawakilishi wa TFF na washirika wa mpango huo. Benki ya NBC iliwakilishwa na Mkuu wa Idara ya Miamala, Bw Mangire Kibanda.
Mhe. Mwinjuma amepongeza hatua hiyo na kutoa wito kwa taasisi mbalimbali nchini kuanzisha siku maalum ambapo wafanyakazi wao wataweza kuvaa jezi za Taifa Stars kama sare rasmi ya kazini.
“Hili ni wazo zuri kwa sababu michezo huleta mshikamano wa kitaifa. Naomba taasisi zizingatie kuwahamasisha na hata kuwanunulia wafanyakazi wao jezi hizi kwa kutumia mfumo huu wa kidijitali,” alisema Mhe. Mwinjuma.
Kwa upande wake, Bw. Kibanda alisema mfumo wa e-commerce wa NBC unawawezesha Watanzania kununua jezi za Taifa Stars bila kufika dukani.
“Unaweza kulipia moja kwa moja kwenye akaunti ya Sunderland ndani ya NBC, au kupitia matawi yetu, mawakala, na huduma za kidijitali kama NBC Kiganjani na NBC Connect,” alifafanua.
Alisisitiza pia umuhimu wa wafanyabiashara kufungua akaunti ya biashara NBC ili kunufaika na malipo kwa njia ya VISA, MasterCard, na njia nyingine za kimataifa.
Uzinduzi huu ni sehemu ya mikakati ya kuendeleza uzalendo, kukuza mauzo ya jezi na kukuza matumizi ya mifumo ya kidijitali nchini.






No comments:
Post a Comment