DAR ES SALAAM - 27 JUNI 2025
SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC) limezindua rasmi huduma ya kusafirisha mizigo kupitia reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR), hatua inayochochea mageuzi makubwa katika sekta ya usafirishaji nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Alhamisi na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa TRC, Fredy Mwanjala, huduma hiyo inaanza kwa treni moja ya mizigo kwa siku.
Treni hiyo yenye jumla ya mabehewa 10 imebeba mizigo mbalimbali ya takribani Tani 700.
Katika ratiba yake, treni hiyo itaondoka Kituo cha Pugu saa 10:00 alfajiri, na kusimama Morogoro saa 12:00 asubuhi kwa ajili ya kupisha treni za abiria, kabla ya kuwasili Dodoma saa 8:05 mchana.
Mwanjala alieleza kuwa TRC inapanga kuongeza idadi ya treni na mabehewa kwa awamu kadri mahitaji yanavyoongezeka ili kukidhi ongezeko la mizigo.
“Shirika linawakaribisha wafanyabiashara, taasisi na wadau wote wa sekta ya usafirishaji kutumia fursa hii ya kisasa, ya haraka na yenye usalama wa hali ya juu kwa ajili ya kuhamisha bidhaa zao,” alisema Mwanjala.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa uzinduzi wa huduma ya mizigo umekuja baada ya mafanikio makubwa ya huduma ya treni za abiria. Tangu kuanzishwa kwake tarehe 24 Juni 2024, zaidi ya wasafiri milioni 2.5 wametumia huduma hiyo hadi kufikia Juni 2025.
Kwa TRC, kuanza kwa usafirishaji wa mizigo ni hatua muhimu inayofungua ukurasa mpya wa matumizi ya SGR katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
👉 Endelea kufuatilia blogu yetu kwa taarifa zaidi kuhusu maendeleo ya miundombinu, usafiri na fursa za kiuchumi nchini Tanzania!
No comments:
Post a Comment