Dodoma, 26 Juni 2025 - Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), kwa kushirikiana na shirika la Africa Community Advancement Initiative (Africai), imezindua rasmi Mradi wa Maji wa Kwadelo katika Wilaya ya Kondoa, Mkoa wa Dodoma – hatua inayoendeleza dhamira ya kampuni hiyo katika kuchochea maendeleo endelevu kupitia upatikanaji wa maji safi na salama vijijini.
Uzinduzi huo ulifanyika Juni 26, 2025, na kuhudhuriwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Mbunge wa Kondoa, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, aliyekuwa mgeni rasmi katika tukio hilo.
Mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi milioni 292 na unatarajiwa kunufaisha zaidi ya wakazi 14,750 wa Kata ya Kwadelo. Utekelezaji wake umehusisha:
- Ufungaji wa pampu ya kisasa ya maji (submersible pump)
- Ujenzi wa nyumba ya mashine
- Tanki la kuhifadhi maji la saruji
- Mtandao wa mabomba ya kusambaza maji
- Vituo 11 vya kuchotea maji vyenye uwezo wa kuzalisha zaidi ya lita 107,000 za maji kwa siku
“Maji ni uhai. Mradi huu unaakisi imani yetu ya dhati kuwa upatikanaji endelevu wa maji ni msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi,” alisema Obinna Anyalebechi, Mkurugenzi Mtendaji wa SBL.
Tangu mwaka 2010, SBL imetekeleza jumla ya miradi 28 ya maji kote nchini, ikitoa huduma ya maji safi kwa zaidi ya Watanzania milioni 2 kupitia mpango wake wa muda mrefu uitwao Water of Life. Mpango huu ni sehemu ya utekelezaji wa vipaumbele vya kampuni katika Mazingira, Jamii na Utawala Bora (ESG), sambamba na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Kwa upande wake, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji aliipongeza SBL kwa mchango wake wa dhati kwa jamii:
“Ushirikiano wa aina hii ndio tunaouhitaji, ambapo sekta binafsi inakuwa sehemu ya kuleta mabadiliko ya kijamii. Maji siyo tu hitaji, bali ni heshima, afya, na fursa kwa jamii,” alisema.
Mradi wa Maji wa Kwadelo unatajwa kuwa mwanzo wa maisha bora na yenye afya kwa maelfu ya wakazi wa Kwadelo na maeneo jirani, huku SBL ikisisitiza kuendelea kushirikiana na wadau wengine katika kusaidia miradi ya maendeleo ya jamii kote nchini.
KUHUSU SBL
Serengeti Breweries Limited (SBL) ilianzishwa mwaka 1988 kama Associated Breweries, na ni kampuni ya pili kwa ukubwa wa uzalishaji wa bia nchini Tanzania. Kwa sasa, inamiliki zaidi ya asilimia 25 ya soko, ikiwa na viwanda vitatu vya uzalishaji vilivyopo Dar es Salaam, Mwanza na Moshi.
Tangu ununuzi wa hisa nyingi na kampuni ya EABL/Diageo mwaka 2010, SBL imewekeza zaidi katika viwango vya kimataifa vya uzalishaji, ikipanua bidhaa zake kila mwaka. Bidhaa zake maarufu ni pamoja na:
- Serengeti Premium Lager
- Serengeti Lite
- Serengeti Lemon
- Pilsner Lager
- Kibo Gold
- Guinness Stout
- Senator
SBL pia inasambaza vinywaji vya kimataifa kama Johnnie Walker, Smirnoff, Gordon Gin, Captain Morgan na Baileys.
Kwa mawasiliano zaidi:
Rispa Hatibu
Meneja Mawasiliano na Uendelevu – SBL
📞 0685 260 901
✉️ Rispa.Hatibu@diageo.com
No comments:
Post a Comment