Aidha, Dkt. Nchemba alitoa wito kwa wananchi na wawekezaji kuchangamkia fursa ya awamu ya pili ya Hatifungani pale itakapozinduliwa rasmi ili kuongeza chachu ya maendeleo kwa taifa letu.
“Napenda kuwahakikishia wawekezaji na wananchi kwa ujumla kuwa Serikali yetu chini ya Uongozi mahiri wa Mama yetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji katika sekta ya fedha na hasa kwenye masoko ya mitaji na dhamana” aliongeza Dkt. Nchemba.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Azania, Dkt. Esther Mang’enya, alisema kuwa hadi sasa jumla ya wawekezaji 650 wamefungua akaunti za CDS kuwawezesha kushiriki katika mauzo ya Bondi Yangu na shughuli zingine za masoko ya mitaji na dhamana ambapo zaidi ya asilimia 97.3 ya wawekezaji walioshiriki katika “Bondi Yangu” ni wawekezaji mmoja mmoja (retail investors).
Aidha, Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam, Bw. Peter Nalitolela, alisema kuwa thamani ya uwekezaji wa hatifungani katika soko hilo imeendelea kuongezeka na sasa imefikia takribani shilingi trilioni 27.6, huku idadi ya wawekezaji ikiwa imefikia 637,137.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama, amepongeza mafanikio hayo, akibainisha kuwa yanatokana na mazingira wezeshi ya uwekezaji yaliyowekwa, ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwa kodi ya zuio kwenye faida ya hatifungani za taasisi.
No comments:
Post a Comment