- Ni kwa kupitia uuzaji wa Hisa za Upendeleo
Mkurugenzi wa Biashara wa Benki ya DCB, Bw. Ramadhan Mganga, akizungumza katika hafla hiyo, jijini Dar es Salaam. |
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa ili kuweza kuhakikisha mtaji wa benki unaendelea kukua mwaka hadi mwaka baada ya zoezi hili na pia kutumiza malengo ya benki, Bodi ya Wakurugenzi iliona ni muhimu kufanya mabadiliko machache ya kiutawala katika menejimenti ya benki yetu, na kumteu Ndugu Sabasaba Moshingi kama Mkurugenzi Mtendaji wa benki mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 20 katika tansia ya benki, huku mabadiliko mengine yakifanyika katika idara ya biashara, mikopo na uendeshaji na teknolojia, idara zote hizi kwa ujumla ni nguzo muhimu katika biashara ya benki.
Alisema uuzaji wa Hisa za upendelo unatarajia kuwaletea wanahisa na watanzania kwa ujumla tija za kiuchumi, baada ya kuongeza mtaji wa benki ambapo unalenga kukuza biashara na kuwapatia wafanyabiashara wadogo wadogo na wa kati mitaji ya kukuza biashara zao na upande mwingine umiliki wa hisa za benki ya DCB unaunga mkono juhudi zinazoendelea za serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi shupavu wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuwaletea watu wake maendeleo.
Bodi ya DCB pamoja na Menejimenti ya benki ilipendekeza na kuidhinisha uuzaji wa Hisa za Upendeleo 97,646,913 zenye thamani ya Shilingi 10,741,160,430 kwa bei ya punguzo ya Shs 110 kwa kila hisa moja, kinyume na Shs 160 iliyopo sokoni, ni matumaini yetu zoezi hii litapata muitikio mkubwa kutoka kwa wanahisa wetu, ambao wana imani na benki hii, bodi na menejimenti yake kwa ujumla.
“Benki imerahisisha ununuzi wa hisa kwa kuruhusu ununuzi kwa njia za kidigitali ili kuongeza wigo wa ushiriki wa wanahisa, natoa rai kwa wanahisa kuchangamkia fursa hii ya kununua hisa kwa njia za kidigitali, au kupitia mawakala wa Soko la Hisa la Dar es Salaam au kwa kufika kwenye matawi yetu ya benki”, aliongeza Bi. Nanyaro.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Masoko na Uchunguzi wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bw. Exaut Julius aliipongeza Benki ya DCB kwa uamuzi huo uliofanyika kwa weledi na ufanisi mkubwa na kupata idhini kutoka CMSA.
Akimwakilisha Ofisa Mtendaji Mkuu wa mamlaka hiyo, CPA Nicodemus Mkama, Bwana Julius alisema, serikali kupitia Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ina jukumu la kuendeleza na kusimamia masoko ya mitaji hapa nchini, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba shughuli katika masoko ya mitaji zinafanyika kwa kufuata sheria, taratibu na miongozo ili kuleta uwazi na haki kwa washiriki wote.
“Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana itaendelea kujenga mazingira wezeshi na shirikishi ili kuwezesha taasisi katika sekta ya umma na binafsi kutumia masoko ya mitaji kupata fedha za kutekeleza miradi na shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuuza hisa kwa umma, hatifungani za miundombinu, hatifungani rafiki za mazingira, hatifungani za bluu, hatifungani za jamii na hatifungani za taasisi za serikali”, alisema Bw. Julius.
Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Sabasaba Moshingi alisema, yeye pamoja na menejimenti yote ya DCB wamejipanga kuhakikisha hadi kufikia Mwaka 2028 wanaandika upya historia ya benki hiyo sambamba na mkakati wa miaka mitano wa maendeleo ya benki hiyo wa kuhakikisha benki inaendelea kukua na kupata faida.
Alisema kwa kuthibitisha hayo, benki hiyo imeweza kutengeneza faida katika robo ya pili na ya tatu huku ikiendelea kutoa huduma za kibenki bila kusahau jukumu la kuanzishwa kwake takribani miaka 22 iliyopita ikiweka mkazo mkubwa katika huduma zake za kidigitali ili kuhakikisha watanzania wengi wanafikiwa na huduma za kibenki.
Tumejipanga kuhakikisha benki yetu inaendeleza maono ya kuanzishwa kwake ambayo ni kusaidia miradi ya kupunguza umasikini kwa kutoa mikopo ya mitaji kwa wajasiriamali wadogo na wa kati waliokosa huduma hizi kutokana na kutokidhi vigezo vya benki ya kibiashara za wakati ule.
“Uuzaji huu wa Hisa za Upendeleo ambao sasa benki yetu inafanya kwa mara ya nne kwa vipindi tofauti utasaidia kuongeza uwezo wa benki yetu katika kuwahudumia wateja wetu na ni imani yetu pia kuanzia mwakani wanahisa wetu wataweza kuanza kupata gawio hivyo tunaomba waendelee kutuunga mkono”, alisema.
No comments:
Post a Comment