Benki ya NMB imesaidia wakulima wa tumbaku zaidi ya 400 mkoani Tabora kulipwa kwa wakati fidia ya hasara waliyopata baada ya mashamba yao kuharibiwa na mvua kubwa za mawe msimu wa 2022/2023. Hundi ya malipo ya madai hayo ya kiasi cha zaidi ya Shilingi milioni 374 kutoka kampuni ya bima ya UAP, imekabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa huo, Balozi Dkt. Batilda Burhani, aliyesema kuwa fidia hizo ni kubwa kuwahi kulipwa wakulima wengi nchini kwa wakati mmoja.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitendo cha Kilimo Biashara wa benki hiyo, Bw. Nsolo Mlozi, amesema Benki ya NMB inaunga mkono juhudi za Serilaki kuhakikisha kilimo nchini kinakuwa na tija na kuwanufaisha wakulima. Hivyo wskishirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Bima (TIRA) wataendelea kuhakikisha wakulima wengi wanapata elimu kuhusu Bima kwani majanga hayatabiriki.
Aidha, alisema mara tu baada ya wakulima hao kufikwa na madhira hayo, Benki ya NMB na Kampuni ya UAP walifanya upembuzi stahiki na tathmini ya kina kuona ni fidia kiasi gani inastahili kwa uharibifu wa mashamba husika na leo wamekabidhi malipo hayo.
Mwakilishi wa UAP, Bi Mariam Hussein, alisema kuwa lengo la kushirikiana na NMB ni kuhakikisha kuwa huduma za bima zinachangia kikamilifu kuendeleza kilimo na kuleta maendeleo ya uchumi nchini. Aliwaasa wakulima ambao hawajakata bima, kutembelea matawi ya NMB nchi nzima kukata bima.
No comments:
Post a Comment