Uzinduzi wa Tawi la NMB Buhigwe uliofanyika chini ya kaulimbiu ya: 'Tunajivunia Kukufikia na Kukuhudumia', umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, ukienda sambamba na makabidhiano ya misaada ya vifaa vya elimu na afya vyenye thamani ya Sh. Milioni 82 kwa shule, hospitali na zahanati za Buhigwe, zikiwemo Shule za Sekondari Kahimba na Nyumbigwa, za Msingi Katema, Nyamiti na Zahanati ya Kasumo zote za mkoani Kigoma.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, ulioshuhudiwa na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Sadat Mussa, Dk. Mpango aliipongeza NMB kwa kuambatanisha tukio hilo na ukabidhi wa vifaa tiba na elimu, sambamba na kulitengea tawi hilo Sh. Bil. 1 ya kukopesha wateja na wadau wa mnyororo wa thamani wa Kilimo na Biashara, huku akiwataka Wana Buhigwe kuzichangamkia.
"Wito wangu NMB na wengine watakaofuata nyayo zenu kuja hapa, hakikisheni elimu ya fedha inawafikia wananchi, wengi wao hapa hawajui maana au faida za hisa na hati fungani. Hawajui umuhimu wa kukopa kwa malengo ndio maana wanaishia kutumia mikopo kwenda kunywea pombe au kuposea wake wa ziada.
"BoT na Umoja wa Mabenki unaweza kuongeza nguvu eneo hilo la elimu ya fedha," alisisitiza Dk. Mpango huku akiitaka NMB yenyewe kuchangamkia fedha za Mfuko wa Mazingira Ili kujiongezea nguvu ya kuimarisha mapambano ya athari za mabadiliko ya tabia nchi kama inavyofanya kupitia Sh. Bilioni 2 ilizotenga kwa ajili ya Kampeni Endelevu ya Upandaji Miti Milioni moja kwa mwaka huu.
Aidha, aliitaka NMB kwamba licha ya uimara na uthabiti wake kimtaji na kiuchumi, inapaswa kujiimarisha na kujiweka kinga zaidi za kudhibiti athari za misukosuko itokanayo na kuyumba kwa Sekta ya Fedha duniani kunatokana na mikwamo kama ya Majanga ya Covid na vita za kimataifa, ambako aliiagiza BoT kuweka mkazo wa kupambana na kuporomoka kwa Mabenki Ili kuyawezesha kuhimiri changamoto hizo kama ilivyo NMB.
Mapema kabla ya Dk. Mpango, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, alisema changamoto ya upotevu wa muda wa kufuata huduma za kifedha mbali imemalizwa, kama zitakavyomalizwa nyingine zilizokwaza ustawi wa kiuchumi wa wakazi wa Buhigwe, ambao wametengewa kupitia tawi lao hilo Sh. Bilioni 1 za mikopo ya kipindi kifupi inayoenda kuongeza thamani ya kilimo hasa kwa mazao ya kimkakati yanayolimwa hapo.
"Tawi limetengewa Sh. Bilioni 1 ya mikopo ya haraka kwa ajili ya kuongeza thamani kwenye mazao ya kimkakati yakiwemo mahindi, pamba, mpunga, kahawa, tangawizi, mihogo, chikichi na mengineyo, pamoja na Biashara na ujasiriamali. Hizi ni sehemu ya jitihada za Kimkakati za NMB kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla," alibainisha Mponzi.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NMB, Dk. Edwin Mhede, alivutiwa na namna Wana Buhigwe walivyohudhuria kwa wingi, akiyaita mahudhurio hayo kama uthibitisho wa utayari na kiu ya huduma za kifedha miongoni mwao na kwamba benki yake iko tayari ikiwa na nguvu za kipesa kukidhi mahitaji ya Wana Kigoma aliowataka wajione kama wamililiki wa hisa za NMB kupitia asilimia 31.8 ya Hisa za Serikali, hivyo kuwasisitiza kuwa NMB ndio chaguo sahihi kwao.
Naye Mkurugenzi wa Usimamizi wa Fedha wa BoT, Sadat Mussa, aliipongeza NMB kwa kusambaza elimu ya fedha na huduma za kibenki mjini na vijijini, na kwamba Sekta hiyo nchini inazidi kuimarika baada ya mkwamo wa Covid na Vita ya Ukraine, ambako jumla ya Sh. Trilioni 29 zimetolewa na taasisi za fedha kama mikopo hadi kufikia Juni mwaka huu, huku BoT yenyewe ikitenga Sh. Trilioni 1 kuyakopesha mabenki hayo.
No comments:
Post a Comment