Foreign Exchange Rates

DStv Advert_090724

DStv Advert_090724

SBT Tanzania Advert_291123

Monday 6 March 2023

SHIRIKA LA BIMA ZANZIBAR LAZINDUA BIMA YA MAGARI KWA WANAWAKE, LAJIVUNIA MAFANIKIO

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima Zanzibar (ZIC), Bw. Arafat Haji (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa hafla fupi ya utambulisho wa huduma mpya ya Bima ya magari mahususi kwa wanawake ijulikanayo kama “Queen Motor Insurance” inayotolewa na Shirika hilo pamoja na uwasilishaji wa taarifa ya mafanikio ya Shirika hilo kwa mwaka 2022. Hafla hiyo imefanyika Zanzibar. Wengine ni watendaji wa Shirika hilo akiwemo Mkurugenzi Idara ya Biashara na Uwekezaji Bw. Mohammed Ameir (wa pili kulia) Meneja wa TEHAMA, Bw. Bakar Yussuf (kulia), Mkurugenzi wa Rasilimali watu Bi. Salma Mwinyi (wa pili kushoto) na Katibu wa Shirika hilo Bi. Asha Rashid (kushoto).

Mkurugenzi wa Rasilimali Watu Shirika la Bima Zanzibar (ZIC), Bi. Salma Mwinyi (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa hafla fupi ya utambulisho wa huduma mpya ya Bima ya magari mahususi kwa wanawake ijulikanayo kama “Queen Motor Insurance” inayotolewa na Shirika hilo pamoja na uwasilishaji wa taarifa ya mafanikio ya shirika hilo kwa mwaka 2022. Hafla hiyo imefanyika Zanzibar. Wengine ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima Zanzibar (ZIC), Bw. Arafat Haji (kulia) na Katibu wa Shirika hilo Bi. Asha Rashid (Kushoto).

Wafanyakazi wa Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) pamoja na wageni waalikwa wakifuatilia hafla hiyo.

Wafanyakazi wa Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) pamoja na wageni waalikwa wakifuatilia hafla hiyo.

Karibu tukuhudumie!

Zanzibar; Machi 6, 2023: Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) limezindua huduma mpya ya Bima ya magari mahususi kwa wanawake ijulikanayo kama “Queen Motor Insurance” huku likijivunia mafanikio makubwa liliyoyapata katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ikiwemo ongezeko la asilimia 169 kwenye mapato yatokanayo na ada za bima (Premiums).

Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa huduma hiyo mpya iliyoambatana na utoaji wa taarifa ya mafanikio ya shirika hilo kwa mwaka 2022, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) Bw. Arafat Haji alisema ujio wa Queen Motor Insurance unalenga kutoa ulinzi na kinga kwa magari binafsi yanayomilikiwa na wanawake endapo yatakabiliwa na majanga mbalimbali ikiwemo ajali, wizi wa gari husika au vipuri pamoja na ajali ya moto.

“Zaidi pia tutahusika na hasara itakayosababishwa na mteja kwa watumiaji wa barabara, pamoja na mali zao kwa kuwa hii ni Bima kubwa,’’ alibainisha.

Kwa mujibu wa Bw. Arafat uzinduzi wa huduma hiyo umekuja wakati huu ikiwa ni ishara ya shirika hilo kuungana na Dunia kuadhimisha siku ya wanawake Duniani na ndio sababu huduma hiyo imeambatana na upendeleo maalum kwa wanawake ikiwemo uanzishwaji wa dawati maalum la kuwahudumia wanawake katika ofisi za shirika hilo kwa huduma za bima na pindi wanapopata ajali.

“Huduma hii itaambatana na malipo ya mafao ndani ya siku saba (7) baada ya kukamilika kwa vielelezo sambamba na faida nyingine nyingi ikiwemo kinga kwa vifaa binafsi kama vile simu na kompyuta, gharama za matibabu ya dharura, malipo yasio na ukomo kwa kioo cha gari, malipo kwa gharama za uvutaji gari wakati wa ajali, mkono wa pole kwa mbima na familia yake na kumpatia mbadala wa usafiri wakati chombo kikiwa katika matengenezo,’’ alitaja.

Akizungumzia mafanikio ya shirika hilo kwa mwaka 2022, Bw. Arafat alisema Shirika limeweza kukusanya mapato yatokanayo na ada za bima (Premiums) kwa kiasi cha sh. 40.2 bilioni sawa na ukuaji wa asilimia 169.55 ikilinganishwa na mapato yaliyokusanywa mwaka uliopita ambapo Shirika hilo lilikusanya kiasi cha Shilingi 23.7 bilioni.

“Tumeweza kufikia asilimia 91 ya malengo yetu kwa mwaka 2022, jambo ambalo linaonyesha ukuaji wetu pamoja na kuzidisha imani kwa wateja wetu waliopo Tanzania nzima. Jumla ya sh 40.2 bilioni zimekusanywa kwa mauzo ya moja kwa moja yaani “ Direct business”, Madalali 14 wa Bima, Mawakala 112, Benki 12 na kupitia mtandao wa simu wa Vodacom ujulikanao kama Vodabima,’’ alitaja.

Alisema mafanikio hayo yameambatana na ukuaji wa uwekezaji wa shirika hilo ambapo kwa mwaka 2022 shirika hilo liliweza kukuza uwekezaji wake kwa asilimia 64.51 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

No comments:

Post a Comment