Mwishoni mwa juma lililopita mchango wa NMB kwenye harakati za kuifanya Tanzania iwe nchi ya uchumi wa kidijitali ulitambuliwa kimataifa na kampuni ya MasterCard International.
Kampuni hiyo kigogo wa teknolojia bunifu duniani iliitunuku NMB tuzo maalum kutambua uwekezaji inayoufanya kusaidia kupunguza matumizi na kutegemea sana pesa taslimu.
NMB ilipewa tuzo hiyo baada ya kuibuka benki kiongozi wa kukuza na kuhamasisha matumizi ya kadi za malipo za MasterCard nchini.
Tuzo hiyo pia inadhibitisha kujitolea kwa NMB kuziimarisha huduma jumuishi za kifedha na kuwa mstari wa mbele kuweka misingi madhubuti ya mifumo ya malipo ya kidijitali.
Nishani iliyopewa NMB na MasterCard Ijumaa jijini Dar es Salaam ni baada ya kufanikiwa kukuza matumizi ya malipo ya kadi kwa kasi kubwa sana.
Katika kufanya hilo, NMB ilivunja rekodi yake yenyewe ya kiasi cha pesa kilichotumika katika vituo vya mauzo kwa kutumia kadi huku thamani ya matumizi hayo ikiongezeka kwa asilimia 30 ndani ya mwaka mmoja.
Kwa mujibu wa MasterCard, ni NMB pekee nchini na katika ukanda huu ambayo imefanikiwa kuongeza matumizi ya kadi za malipo kwa zaidi ya asilimia 100 katika kipindi cha miezi 12.
Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa benki hiyo, Bw. Filbert Mponzi, alisema mafanikio yaliyoifanya NMB kuibuka kidedea yalipatikana kati ya Juni 2020 na Juni 2021.
“Tuzo hii ni kielelezo tosha kabisa cha ukubwa wa Benki ya NMB nchini inayochagizwa na upana wa mtandao wake wa matawi 226 na wateja zaidi ya milioni nne,” kiongozi huyo alinena kabla ya kupokea tuzo ya MasterCard.
“Hii ni tuzo ya kwanza ya namna hii kuwahi kutolewa kwa benki hapa nchini Tanzania. Asanteni sana wenzetu wa MasterCard na pia shukrani nyingi kwa wateja wa NMB waliotufanya kutambuliwa na MasterCard,” Bw. Mponzi alisema.
Sababu zilizopelea ushindi huu wa kidijitali wa NMB ni mbili. Kwanza ni idadi kubwa zaidi ya wateja wanaotumia kadi kuliko benki yoyote nchini. Zaidi ya wateja wa NMB milioni tatu wanatumia kadi za MasterCard kwa ajili ya huduma mbalimbali za kifedha idadi ambayo haijafikiwa na benki nyingine zote nchini.
Bw. Mponzi alisema sababu ya pili ni kiasi kikubwa cha pesa kilichotumika katika vituo vya malipo kwa kutumia kadi za NMB MasterCard ambacho kiliongezeka kwa asilimia 104 ndani ya mwaka mmoja.
“Mbali na sababu hizi, Benki ya NMB imekuwa kinara katika kuhamasisha matumizi ya kadi sio tu kwa ajili ya kutolea pesa katika ATM bali na katika matumizi mengine mengi kama kufanya malipo katika sehemu za migahawa, supermarket, vituo vya mafuta na katika sehemu za starehe na hata kuagiza bidhaa mbalimbali kupitia mitandao.”
Bw Mponzi alisema kutambuliwa mchango wa NMB kwenye mafanikio ya nchi kidijitali ni sifa nyingine ya taasisi hiyo kutokuwa na mpinzani sokoni na tuzo ya Mastercard ni moja ya nyingi za ubora ilizotunukiwa mwaka huu.
Aidha, alisema NMB pia ni mahili katika maeneo mengine kama kuongoza kupata faida pamoja na kuwa na kiasi kikubwa cha amana na rasilimali fedha.
Ili kuendeleza uongozi huo, Bw Mponzi aliweka wazi mikakati ya NMB kwa ajili ya hilo akisisitiza kuepukana na ubaili kwenye uwekezaji na umuhimu wa ubunifu.
“Benki ya NMB itaendelea kubuni suluhisho mbalimbali zenye lengo la kuboresha matumizi ya kadi na kwa kutumia teknolojia mbalimbali,” alibainisha
“Ni imani yetu kuwa idadi ya watumiaji wa kadi itazidi kuongezeka na hata miamala kupitia kadi itaongezeka zaidi,” aliongeza na kuisifia Mastercard kwa ubobezi wake katika teknolojia ya kadi za malipo.
Mwaka 2014, NMB na Mastercard walikubaliana kushirikiana kutumia malipo ya kielektroniki kuchochea uchumi wa kidijitali na kuwa sehemu ya ajenda ya taifa ya kufanikisha huduma jumuishi za kifedha.
Meneja wa MasterCard Afrika Mashariki, Bw Shehryar Ali, alisema tuzo ya NMB ni zaidi ya kuwezesha matumizi ya kadi kwani benki hiyo imefanya mengi kusaidia kupunguza matumizi ye pesa taslimu na kuendeleza huduma za kifedha nchini.
“Matumizi ya pesa taslimu ambayo yanafikia hadi asilimia 90 ya miamala yote inayofanyika Tanzania yanaughalimu uchumi wa nchi asilimia mbili za pato la taifa kwa sababu lazima pesa hizo zichapishwe, zihifadhiwe, zisafirishwe na zilindwe,” Bw Ali alifafanua.
No comments:
Post a Comment