Kampuni ya Tanga Cement (TCPLC) imetangaza kupata faida ya uendeshaji ya shilingi za Kitanzania Bilioni 14.9 kwa kipindi cha mwaka kinachoishia Disemba 31, 2018 kutoka hasara iliyotokana na uendeshaji ya shilingi Bilioni 10.99 kwa Mwaka 2017.
Akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa wanahisa wa Kampuni hiyo Jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya Tanga Cement, Lau Masha alisema pia kuwa utendaji wa mwaka 2018 umesaidia kupunguza hasara baada ya kodi ya shilingi billion 11.3 kutoka shilingi bilioni 26.3 kwa mwaka 2017. “Mauzo ya kundi letu yalipanda kwa 25% na kufika shilingi bilioni 214.9 kutoka shilini bilioni 171.8 zilizopatikana kwa mwaka uliopita wakati faida ghafi kwa mwaka iliongezeka kwa 91% na kuwa shilingi bilioni 56.2 kutoka shilingi bilioni 29.4 zilizopatikana mwaka uliopita,” alisema.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa ukuaji wa biashara ulijikita katika ukuuaji wa simenti na secta ya ujenzi nchini Tanzania. Matumaini miundombinu chini ya mipango ya dira ya maendeleo ya serikali ya mwaka 2025
Pamoja na hayo mwenyekiti huyo alisema kutokana na Tanzania kuwa soko la pili kwa ukubwa kwa masuala ya ujenzi Afrika Mashariki, uzalishaji wa simenti unatarajiwa kuongezeka hivyo Kampuni yao imejipanga kuhakikisha inanufaika na ukuaji huo katika soko la Kanda.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Reinhardt Swart alisema, kampuni iliongeza uzalishaji kwa kipindi chote hiki cha mwaka na kuweza kuzalisha mapato ya ziada kutokana na mauzo ya klika ya ziada iliyozalishwa.
Mkurugenazi huyo aliongeza kuwa mkataba wao na Kampuni ya reli Tanzania (TRC) umewawezesha kupata mabehewa zaidi ambayo yapo kwa ajili ya usafirishaji katika maeneo yao ya kimikakati ya usambazaji. Unafuu huo unapunguza gharama za kuhifadhi na usafirishaji huku ukuupa nguvu usafiri wa reli na usambazaji nchini Tanzania
“Ingawa kushuka kwa thamani ya fedha na riba tunayolipa kutokana na mkopo tuliochukua kwa ajili ya mtaji wa uwekezaji mpya wa kinu namba mbili (TK2) vimeendelea kubakia kuwa matumizi ya gharama kubwa, hasara baada ya kodi kwa mwaka 2018 ilipungua,” aliongeza Mkurugenzi huyo.
Pamoja na mafanikio hayo kampuni haikutangaza gawio la mpito kwa wanahisa wake kwa mwaka 2018 kutokana sababu zilizoelezwa mahali hapo kuwa ni hali iliyotokana na utendaji wake wa kifedha kwa mwaka 2017 hivyo bodi kuamua kutumia busara kutotangaza gawio la mwisho ili fedha iliyopo kutumika katika shughuli za utendaji na kulipia madeni.
No comments:
Post a Comment