Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Fedha wa Coca Cola Kwanza, Erastus Mtui, Mkuu wa Kitengo cha Ugavi (Vifaa) Pankaj Singh, Meneja Masoko na Mauzo Bi. Josephine Msalilwa na Haji Ally Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Matukio ya Kijamii wakionyesha kinywaji kipya kilichozinduliwa cha Schweppes +C hivi karibuni jijini Dar es salaam. |
Mkuu wa Kitengo cha Fedha wa Coca Cola Kwanza, Erastus Mtui, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kwenye uzinduzi wa kinywaji kipya cha Schweppes +C cha kampuni ya Coca Cola Kwanza. |
Dar es salaam. Kampuni ya vinywaji baridi ya Coca-Cola Tanzania, imezindua kinywaji kipya chenye ladha ya limao kinachojulikana kama Schweppes +C, ikiwa ni sehemu ya kuongeza machaguo ya bidhaa kwa wateja wake.
Kinywaji cha Schweppes +C kinawalenga zaidi wateja wenye umri mkubwa.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa kinywaji hicho jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Coca Cola, Basil Gadzios, alisema kampuni yake imewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye ugunduzi na kuongeza idadi ya bidhaa tofauti tofauti ikiwa na lengo la kukidhi mahitaji ya wateja tofauti tofauti katika soko la Tanzania.
Tunayo furaha kuongeza bidhaa nyingine mpya sokoni ikiwa ni shehemu ya jitihada za kukidhi mahitaji ya wateja wetu. Schweppes +C yenye ladha ya limao inawaletea wateja wetu ladha ya kipekee ya limao ikiwa na Vitamini C ambayo tunaamini wataifurahia.
Kinywaji kimetengenezwa mahususi kumpa mtumiaji wake ladha nzuri ya juisi ya limao.
Tukiwa kama kampuni ya vinywaji baridi, tumejidhatiti kuwaletea wateja wetu kilicho bora na bado tuna vingi kwa ajili yao, alisema mkurugenzi huyo.
Gadzios aliongeza kuwa, Coca-Cola inatarajia kuingiza sokoni bidhaa nyingine nyingi ambazo siyo tu zitakidhi mahitaji ya jamii ya leo bali pia zitaendana na wateja ambao mahitaji yao hubadilika katika soko la kileo huku akiongeza kuwa kinywaji hicho kipya kimetengenezwa kwa kuzingaatia viwaango vyaa kimataifa kikiwa na ladha ya kipekee ya limao.
“Kuwashirikisha wateja wetu, ni moja kati ya vipau mbele vya kampuni ya Coca-Cola. Hii inatusaidia kuyafahamu mahitaji yao ambayo hubadilika kulingana na muda na hivyo kutuwezesha kuwatengenezea bidhaa zinazoendana na mahitaji na matakwa yao kwa kuwashirikisha.
Kuongezwa kwa Vitamin C kwenye kinywaji kipya cha Schweppes +C, kunakifanya kinywaji hiki kitofautiane na vinywaji vyetu vingine vilivyopo sokoni huku kikiwapa wateja ladha murua ya limao, alieleza.
Kinywaji cha Schweppes +C kitauzwa kwa shilingi 1,000 kwa bei ya reja reja bei ambayo itawawezesha wateja kuweza kukifurahia.
No comments:
Post a Comment