TAASISI ya kifedha ya Bayport Financial Services inayojihusisha na mambo ya mikopo imepongezwa na serikali kwa hatua yake ya kufungua tawi wilayani Kwimba mkoani Mwanza.
Shughuli za uzinduzi huo zilifanyika Machi 2 mwaka huu, huku mgeni rasmi akiwa ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Kwimba, Vicent Emmanuel, akiongozana na viongozi mbalimbali wa serikali wilayani humo.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Katibu Tawala huyo wa wilaya Kwimba, Emmanuel alisema kwamba kufunguliwa kwa tawi hilo kutatoa huduma karibu na wananchi, kama njia ya kukuza uchumi wao kwa ujumla, zikiwapo fursa za kukopeshwa bidhaa mbalimbali, vikiwamo vyombo vya usafiri.
Alisema kwamba awali watu wa Kwimba walilazimika kusafiri umbali mrefu kupata huduma za mikopo, lakini sasa wamesogezewa huduma karibu, hivyo ni jukumu lao kutumia fursa hiyo kwa ajili ya kujinufaisha kwa ajili ya maisha yao.
“Serikali tunaipongeza Bayport Financial Services kwa hatua ya kuanzisha tawi hapa Kwimba, hivyo tunaamini kwa pamoja tutafanikisha maendeleo kwa watu wote kwa kupitia njia ya mikopo kwa watumishi wa umma na wafanyakazi waliodhinishwa,” alisema Emmanuel.
Naye Meneja Mauzo wa Bayport Financial Services Kanda ya Ziwa, Lugano Kasambala, alisema kwamba tawi lao limejipanga kutoa huduma bora kwa wakazi na wananchi wa Kwimba waliokuwa wakisafiri umbali mrefu kupata huduma zao.
“Huu ni mwendelezo wa Bayport Financial Services kuhakikisha kwamba tunaendelea kufungua matawi katika sehemu mbalimbali, ambapo sasa tumefikisha matawi 79 nchini kote, ambapo uwapo wa taasisi yetu umerahisisha maisha kwa watumishi wa umma na wafanyakazi waliodhinishwa na taasisi yetu.
“Tunaomba wachangie fursa za mikopo mbalimbali kama ile ya bidhaa, mikopo ya fedha, bima ya elimu kwa uwapendao, ambapo katika mikopo ya bidhaa, mteja anaweza kukopeshwa bodaboda, vifaa vya ujenzi, injini za boti, pembejeo za kilimo na huduma nyingine nzuri na muhimu kwa Watanzania wote,” alisema.
Kwa mujibu wa Kasambala, huduma za Bayport ni rahisi kupatikana ndani ya saa 24, huku zikiwa hazina amana wala dhamana, jambo linaloonyesha mafanikio makubwa kwa wateja wetu watakaoamua kupata huduma katika taasisi yao.
Bayport Financial Services ni taasisi inayojihusisha na mikopo, huku ikiwa na matawi katika mikoa mbalimbali ya Tanzania, ambapo kwa kupitia tawi la Kwimba, wateja wao hawatalazimika kusafiri ili wapate huduma za taasisi hiyo.
Jiachie Blog
No comments:
Post a Comment