Blog Rebranding Teaser_030826

Blog Rebranding Teaser_030826

Absa Banner_301026_111126

Stanbic Bank Banner_201026

Monday, 16 November 2026

NMB YAWAHIMIZA WATANZANIA KUWEKA AKIBA KWA MALENGO, KUJENGA MITAJI YA MUDA MREFU

DODOMA - Novemba 16, 2026: Benki ya NMB imewahimiza Watanzania kujenga utamaduni wa kuweka akiba kwa malengo na kufanya maamuzi sahihi ya uwekezaji ili kuimarisha ustawi wao wa kifedha na kujenga mitaji kwa ajili ya maendeleo ya muda mrefu.

Wito huo umetolewa katika warsha ya From Saving to Smart Investing (Akiba Hadi Uwekezaji) iliyoandaliwa na Bridge Consult kwa udhamini wa NMB, iliyofanyika katika Ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma.

Akizungumza katika warsha hiyo, Mkuu wa Idara ya Uhusiano na Wawekezaji wa NMB, Mark Hiza, aliwahimiza wananchi kutathmini hali zao za kifedha na kuweka malengo ya kifedha ya muda mfupi na mrefu, yakiwemo ya miaka mitatu, mitano na kumi.

Alieleza kuwa kupanga malengo ya kifedha ni hatua muhimu katika kujenga nidhamu ya matumizi, kuweka akiba na kujiandaa kwa fursa za uwekezaji zitakazowasaidia kujenga mitaji.

Hiza alibainisha kuwa kupitia huduma ya kidijitali ya NMB Mkononi, wateja wanaweza kusimamia akaunti zao na kufanya miamala kwa urahisi. Aidha, vikundi vya kuweka na kukopa (Vikoba) vinawezeshwa kufungua na kusimamia akaunti kidijitali, hatua inayosaidia kuimarisha usalama na uwazi katika usimamizi wa fedha za vikundi.

Kwa upande wake, Meneja Mwandamizi wa Huduma za Kibenki kwa Wateja Binafsi wa NMB, Zuberi Bani, alisisitiza umuhimu wa elimu ya fedha, hususan kwa vijana, ili waweze kupanga matumizi yao, kuweka akiba na kutumia huduma za kifedha za kidijitali kwa usalama.

Alitaja akaunti ya NMB Kikundi na mpango wa Go na NMB kuwa miongoni mwa suluhisho zinazotumiwa na benki hiyo kuwafikia wananchi, kuwajengea nidhamu ya kifedha na kuwawezesha kutumia huduma za kibenki katika kujiendeleza kiuchumi.

Ushiriki wa NMB katika warsha hiyo ni sehemu ya juhudi za benki hiyo za kukuza elimu na ujumuishaji wa kifedha nchini, kwa kuhamasisha Watanzania kutumia huduma rasmi za kibenki, kuweka akiba kwa malengo na kujenga msingi imara wa uwekezaji wa muda mrefu.

Kupitia elimu ya fedha na suluhisho mbalimbali za kibenki, NMB inaendelea kuhamasisha wananchi kuona akiba siyo tu fedha zinazotengwa kwa matumizi ya baadaye, bali pia ni msingi muhimu wa kujenga mitaji na kufikia malengo ya maendeleo ya kifedha.





No comments:

Post a Comment