Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, atembelea banda la NMB katika Mkutano wa Madini na Uwekezaji Tanzania 2026 na kupata maelezo kuhusu huduma za kifedha zinazolenga wachimbaji na wadau wa sekta hiyo.
Dar es Salaam | November 20, 2026
Benki ya NMB imeendelea kuonesha dhamira yake ya kusaidia ukuaji wa sekta ya madini nchini kwa kutoa suluhisho mbalimbali za kifedha zinazolenga kuwawezesha wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa pamoja na wafanyabiashara wanaoshiriki katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.
Dhamira hiyo imebainishwa wakati Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, alipotembelea banda la Benki ya NMB katika Mkutano wa Madini na Uwekezaji Tanzania 2026, unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo, Makamu wa Rais alipokelewa na Mkuu wa Idara ya Miamala wa Benki ya NMB, Linda Teggisa, ambaye alimweleza kuhusu huduma na masuluhisho mbalimbali ya kifedha yanayotolewa na benki hiyo kwa ajili ya kusaidia shughuli za uchimbaji madini na biashara zinazohusiana na sekta hiyo.
Huduma zilizoangaziwa ni pamoja na mikopo kwa wachimbaji, huduma za miamala na malipo pamoja na masuluhisho ya kibenki ya kidijitali yanayolenga kurahisisha shughuli za kifedha, kuongeza ufanisi wa biashara na kuwawezesha wadau wa sekta ya madini kupanua shughuli zao.
Kupitia huduma hizo, NMB inalenga kuchangia upatikanaji wa mitaji na huduma rasmi za kifedha kwa wadau wa sekta ya madini, ambao wanahitaji rasilimali za kifedha ili kuwekeza katika shughuli zao na kuongeza uwezo wa uzalishaji.
Ushiriki wa NMB katika Mkutano wa Madini na Uwekezaji Tanzania 2026 unaonesha nafasi ya taasisi za kifedha katika kuchochea uwekezaji na kuimarisha sekta ya madini, ambayo ni miongoni mwa sekta muhimu zinazochangia uzalishaji, ajira, mapato ya taifa na ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Kwa kuendelea kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya wadau wa sekta hiyo, NMB inalenga kuwa sehemu ya safari ya kukuza uwekezaji na kuimarisha mchango wa sekta ya madini katika maendeleo ya uchumi wa nchi.


.jpeg)
.jpeg)
No comments:
Post a Comment