Blog Rebranding Teaser_030826

Blog Rebranding Teaser_030826

Stanbic Bank Banner_070826

Stanbic Bank Banner_070826

Absa Loan Campaign_160426

Absa Loan Campaign_160426

Wednesday, 9 September 2026

NMB YAWEKA SH. MILIONI 165 KUSUKUMA MAUZO KARIAKOO, YAPANUA MALIPO YA KIDIJITALI KARIAKOO FESTIVAL 2026

Mkuu wa Idara ya Biashara wa Benki ya NMB, Alex Mgeni (kushoto), akionesha namna ya kulipia bidhaa kupitia NMB Mkononi wakati wa uzinduzi wa Kariakoo Festival 2026 jijini Dar es Salaam. Wanaoshuhudia ni Mkurugenzi Mtendaji wa One Voice Events na Mratibu wa tamasha hilo, George Lupenza (katikati), pamoja na Mkuu wa Ubunifu na Mikakati wa Clouds Media Group, Reuben Ndege (kulia).
Mkuu wa Idara ya Biashara wa Benki ya NMB, Alex Mgeni, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kariakoo Festival 2026 jijini Dar es Salaam. Alisema tamasha hilo litatumika kuongeza fursa za mauzo kwa wafanyabiashara na kupanua matumizi ya malipo ya kidijitali.

DAR ES SALAAM | Septemba 9, 2026

Wafanyabiashara wa Kariakoo wanatarajiwa kupata fursa zaidi za kuongeza mauzo na kupokea malipo kwa njia za kidijitali kupitia msimu wa tatu wa Kariakoo Festival 2026, baada ya Benki ya NMB kutangaza udhamini wa Shilingi milioni 165 kwa ajili ya tamasha hilo.

Tamasha hilo lenye kaulimbiu “Bei Shwaa Shwaa” litafanyika kuanzia Septemba 25 hadi 27, 2026, katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, likiwakutanisha wafanyabiashara na wanunuzi kwa siku tatu za mauzo ya bidhaa kwa bei za punguzo.

Msimu wa tatu wa Kariakoo Festival ulizinduliwa Septemba 8, 2026, kwa msafara maalumu wa wafanyabiashara ulioanzia Viwanja vya Mnazi Mmoja na kupita Barabara za Lumumba na Uhuru pamoja na mitaa ya Msimbazi na Mkunguni, kabla ya kuishia katika Soko Kuu la Kariakoo.

Uzinduzi huo uliongozwa na Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo, Ashraph Abdulkarim, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo. Viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo na waandaaji wa tamasha hilo pia walishiriki.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Idara ya Biashara wa NMB, Alex Mgeni, alisema benki hiyo inalenga kutumia tamasha hilo kupanua soko la wafanyabiashara na kuongeza matumizi ya njia salama za malipo zinazopunguza utegemezi wa fedha taslimu.

“NMB tunataka kuwapo kila pale ambapo biashara ipo. Tunataka kuona wafanyabiashara wa Kariakoo, Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla wakikua pamoja na biashara zao,” alisema Mgeni.

MALIPO YA KIDIJITALI

Mgeni alisema wakati wa tamasha hilo, wafanyabiashara watapata huduma za kupokea malipo kupitia NMB Lipa Namba na NMB Mkononi.

NMB pia itaonesha matumizi ya NMB Tap, teknolojia inayowezesha malipo kwa kutumia vifaa kama pete, bangili au stika kwenye vituo vinavyokubali malipo ya kugusa.

Kwa mujibu wa Mgeni, mifumo hiyo itawarahisishia wafanyabiashara kuhudumia wanunuzi kwa haraka na kuweka kumbukumbu za miamala yao, hasa katika kipindi ambacho tamasha linatarajiwa kuvutia idadi kubwa ya wateja.

FURSA ZA MIKOPO

Mbali na huduma za malipo, NMB itatumia Kariakoo Festival kuwafikishia wafanyabiashara taarifa kuhusu fursa za mikopo kwa ajili ya kuongeza mtaji na kukabiliana na mahitaji ya muda mfupi ya fedha.

Wateja wanaokidhi vigezo wanaweza kupata Mshiko Fasta wa hadi Shilingi milioni mbili kwa mtu binafsi na hadi Shilingi milioni tano kwa mfanyabiashara kupitia NMB Mkononi, kulingana na kikomo kilichoidhinishwa.

Aidha, NMB SME World Business Credit Card inawawezesha wafanyabiashara wanaostahili kupata mkopo wa hadi Shilingi milioni 50 na muda wa hadi siku 53 bila riba kwa miamala inayokidhi masharti.

Taarifa kuhusu mikopo ya vifaa vya kazi, mashine, mitambo pamoja na biashara za usambazaji wa nishati safi ya kupikia pia zitatolewa wakati wa tamasha hilo.

KARIAKOO YAREJEA KWA NGUVU

Kwa upande wake, Abdulkarim alisema tamasha la mwaka huu linafanyika baada ya kukamilika kwa ujenzi na ukarabati wa Soko Kuu la Kariakoo, lililoathiriwa na moto.

Alisema wafanyabiashara na wanunuzi watapata nafasi ya kuona vizimba, maeneo ya biashara na huduma mbalimbali zinazopatikana katika soko hilo.

“Lengo ni kuhakikisha wafanyabiashara wanauza kwa bei nafuu na kupunguza bidhaa zilizopo maghalani kuelekea mwisho wa mwaka,” alisema Abdulkarim.

Aliwataka wafanyabiashara kujisajili mapema na wanunuzi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika tamasha hilo.

NMB YAWEZESHA MSIMU WA TATU

Mkurugenzi Mtendaji wa One Voice Events na Mratibu wa Kariakoo Festival, George Lupenza, alisema udhamini wa NMB umewezesha tamasha hilo kuendelea kwa msimu wa tatu na kulifikisha kwa wafanyabiashara wengi zaidi.

Kwa siku tatu, Kariakoo Festival 2026 itawapa wafanyabiashara soko la moja kwa moja la bidhaa zao, huku ikiweka msisitizo katika matumizi ya malipo ya kidijitali.

Waandaaji wamewataka wafanyabiashara kukamilisha usajili mapema ili kunufaika na fursa zitakazotolewa wakati wa tamasha hilo.

Endelea kufuatilia Kitomari Banking & Finance Blog kwa habari zaidi kuhusu biashara, benki, fedha, uwekezaji na maendeleo ya sekta mbalimbali nchini Tanzania.





No comments:

Post a Comment