Blog Rebranding Teaser_030826

Blog Rebranding Teaser_030826

Stanbic Bank Banner_070826

Stanbic Bank Banner_070826

Absa Loan Campaign_160426

Absa Loan Campaign_160426

Tuesday, 8 September 2026

MASHINDANO YA VODACOM CORPORATE MASTERS GOLF YAMALIZIKA KWA MAFANIKIO, YAIMARISHA MAHUSIANO YA KIBIASHARA

Washindi wa Vodacom Corporate Masters Golf Tournament 2026 katika makundi mbalimbali wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukabidhiwa zawadi zao katika hafla iliyofanyika Lugalo Golf Club, Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki.
Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando (kulia), akikabidhi tiketi ya kwenda na kurudi Mauritius kwa mshindi wa jumla kwa upande wa wanaume, Khalid Shemndolwa (wa tatu kushoto), katika Vodacom Corporate Masters Golf Tournament 2026, iliyofanyika Lugalo Golf Club, Dar es Salaam.

Dar es Salaam, Septemba 5, 2026: Vodacom Tanzania PLC, kwa kushirikiana na Oakwood Holdings Limited, imehitimisha kwa mafanikio mashindano ya Vodacom Corporate Masters Golf 2026, yaliyofanyika katika Uwanja wa TPDF Lugalo Golf Club jijini Dar es Salaam.

Mashindano hayo yaliwakutanisha takribani wachezaji 150 kutoka Tanzania na nchi jirani, wakiwemo viongozi wa biashara, wakurugenzi, wakuu wa kampuni pamoja na wapenzi wa mchezo wa gofu.

Katika mashindano hayo ya siku moja, Khalid Shemndolwa na Yvonne Ondari waliibuka washindi wa jumla kwa upande wa wanaume na wanawake, mtawalia. Shemndolwa alikusanya pointi 42, huku Ondari naye akifikisha pointi 42.

Katika madaraja mengine, Godfrey Abel alitwaa ubingwa wa Daraja A baada ya kupata pointi 42, akifuatiwa na Likuli Juma aliyemaliza na pointi 41.

Kwa upande wa Daraja B, Sigfrid Urassa aliibuka mshindi kwa pointi 40, akimzidi Godfrey Kilenga, ambaye pia alipata pointi 40, lakini Urassa akashinda kwa kutumia kanuni ya countback.

Boniface Japhet alitwaa ubingwa wa Daraja C baada ya kupata pointi 39, huku Abdallah Singano akimaliza nafasi ya pili kwa pointi 37.

Kwa upande wa wanawake, Neema Job alitwaa ubingwa baada ya kupata pointi 42, akifuatiwa na Leticia Kapalia, aliyepata pointi 40.

Mashindano ya timu za kampuni nayo yalikuwa sehemu muhimu ya tukio hilo, ambapo timu ya KQ iliibuka mshindi baada ya kushindana dhidi ya timu nyingine tisa za kampuni.

Katika tuzo maalum za mtu mmoja mmoja, Michael Norbert alishinda tuzo ya Longest Drive kwa wanaume, huku Leticia Kapalia akitwaa tuzo hiyo kwa upande wa wanawake.

Kwa upande wa Nearest to the PinHarshid Barmeda alishinda kwa wanaume, wakati Vaileth James alitwaa tuzo hiyo kwa wanawake.

CORPORATE VILLAGE YAWA KIVUTIO

Mbali na ushindani wa gofu, washiriki pamoja na familia zao walipata fursa ya kufurahia shughuli mbalimbali katika eneo la Corporate Village, lililokuwa na burudani, maonesho ya biashara, magari ya zamani pamoja na eneo maalum kwa ajili ya watoto.

Akizungumza kuhusu mashindano hayo, Mkurugenzi wa Vodacom Business wa Vodacom Tanzania PLC, Nguvu Kamando, alisema tukio hilo limeendelea kuonyesha umuhimu wa michezo katika kujenga na kuimarisha mahusiano yenye tija katika sekta ya biashara.

“Vodacom Corporate Masters 2026 Golf Cup imethibitisha tena kwamba michezo ni jukwaa lenye nguvu katika kujenga mahusiano ya muda mrefu ya kibiashara. Tunafurahishwa na ushiriki mkubwa wa kampuni na kasi ya mahusiano mapya yaliyojengwa wiki hii,” alisema Kamando.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Corporate Masters, Ken Kariuki, alizipongeza kampuni zilizoshiriki na kusema mashindano hayo yanaendelea kuwa jukwaa muhimu la kujenga mitandao ya kibiashara na kukuza mchezo wa gofu.

“Mwaka huu tulishuhudia ushindani wa kiwango cha juu uwanjani na ushiriki wenye maana katika biashara nje ya uwanja. Hilo ndilo lengo kuu la Corporate Masters—kuzikutanisha kampuni katika mazingira rafiki yanayozalisha fursa halisi za ushirikiano,” alisema Kariuki.

Kariuki aliongeza kuwa ushirikiano kati ya Vodacom na Corporate Masters unaonyesha namna kampuni zinavyoweza kufanya kazi pamoja katika kutengeneza thamani kwa wateja na wadau, huku zikiunga mkono maendeleo ya mchezo wa gofu nchini Tanzania.

MICHEZO KAMA JUKWAA LA BIASHARA

Kufanikiwa kwa mashindano ya Vodacom Corporate Masters Golf 2026 kunaendelea kuonyesha nafasi ya michezo kama jukwaa la kuimarisha mahusiano ya kibiashara na kuunganisha viongozi wa kampuni katika mazingira yanayochochea mazungumzo, mitandao na fursa mpya za ushirikiano.

Kwa Vodacom Tanzania, mashindano hayo pia yanaendana na juhudi za kampuni kutumia majukwaa mbalimbali kuwaunganisha wafanyabiashara na suluhisho za kidijitali zinazolenga kuongeza ufanisi wa biashara na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Mshindi wa jumla kwa upande wa wanawake, Yvonne Ondari (wa tatu kushoto), akipokea zawadi baada ya kutwaa taji katika Vodacom Corporate Masters 2026 Golf Tournament.
Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando, akishiriki mashindano ya Vodacom Corporate Masters 2026 Golf Cup.

Mkuu wa Idara ya Masoko na Uwezeshaji wa Vodacom Business, Joseph Sayi, akishiriki mashindano ya Vodacom Corporate Masters 2026 Golf Cup.

Kitomari Banking & Finance Blog itaendelea kukuletea habari na taarifa muhimu kutoka katika sekta ya biashara, benki, fedha na uchumi nchini Tanzania. Endelea kutufuatilia.

No comments:

Post a Comment