Dar es Salaam, Septemba 7, 2026: Benki na taasisi nyingine za fedha zinazojihusisha na utoaji wa mikopo sasa zitaweza kubaini kwa urahisi zaidi wakopaji wasio waaminifu wanaotumia mbinu mbalimbali kuficha taarifa zao halisi ili kujipatia mikopo kwa njia za udanganyifu.
Hayo yamekuja kufuatia kuzinduliwa kwa mfumo mpya unaojulikana kama Fraud and ID Solution, uliozinduliwa na kampuni ya Creditinfo Tanzania, ambao unalenga kusaidia taasisi za fedha kuthibitisha utambulisho wa wateja kabla ya kutoa mikopo.
Mfumo huo utawezesha taasisi za fedha kumtambua mteja anayehitaji mkopo na kubaini iwapo anatumia majina, nyaraka au utambulisho ambao si wake au si halali.
BENKI KUU YA TANZANIA YAUPONGEZA MFUMO
Akizungumza katika uzinduzi wa mfumo huo, Bw. Deogratias Mnyamani kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) alisema huduma hiyo itazisaidia taasisi za fedha nchini kupambana na udanganyifu unaohusiana na mikopo, huku ikichangia kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa wakopaji waaminifu.
Alisema kwa miaka mingi huduma za aina hiyo zimekuwa zikitolewa na kampuni za kimataifa zilizopo nje ya Tanzania.
“Leo tunaondokana na kutegemea huduma hii muhimu kutoka kwa makampuni yaliyopo nje ya nchi yetu. Hii ni mara ya kwanza huduma hii inatolewa na kampuni iliyopo hapa hapa Tanzania ambayo ina uelewa mpana wa soko letu, taasisi zetu za kifedha na watu wetu. Nawapongeza sana Creditinfo kwa kuja na huduma hii,” alieleza Bw. Mnyamani.
MABADILIKO YA KIDIJITALI YAMEONGEZA HATARI YA FRAUD
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Creditinfo Tanzania, Bw. Edwin Urasa, alisema mabadiliko makubwa katika sekta ya fedha, ambayo yamechochea upanuzi wa huduma za kibenki pamoja na mifumo mbalimbali ya malipo ya kidijitali, yameongeza pia changamoto ya udanganyifu wa kifedha.
Alisema kupitia Fraud and ID Solution, Creditinfo inatumia taarifa kutoka mamlaka mbalimbali kusaidia taasisi za fedha kuthibitisha iwapo utambulisho unaowasilishwa na mkopaji ni halali kabla ya taasisi kufanya uamuzi wa kutoa mkopo.
“Uaminifu ni jambo muhimu sana, hasa katika kipindi hiki ambacho taasisi zinafanya mawasiliano na wateja kwa njia ya kidijitali pasipo kulazimika kuonana. Kumjua kwa uhakika yule unayewasiliana naye ni muhimu katika kulinda biashara na wateja wake pia,” alisema Bw. Urasa.
Alifafanua kuwa huduma hiyo mpya inazipatia taasisi za fedha taarifa za kiintelijensia kuhusu wateja, jambo linaloweza kusaidia katika kufanya maamuzi sahihi zaidi wakati wa mchakato wa utoaji wa mikopo.
“Huduma hii mpya inazipatia taasisi za kifedha taarifa za kiintelijensia kuhusu mteja ili kuweza kufanya maamuzi yenye tija,” aliongeza.
MFUMO WALAENGA KUIMARISHA UAMINIFU KATIKA UKOPESHAJI
Uzinduzi wa Fraud and ID Solution unakuja wakati taasisi za fedha zikiendelea kuongeza matumizi ya teknolojia katika huduma za kifedha, ikiwemo utoaji wa mikopo na huduma nyingine zinazoweza kutolewa bila mteja na mtoa huduma kukutana ana kwa ana.
Kwa kutumia mfumo huo, taasisi za fedha zinalenga kuimarisha mchakato wa kumtambua mteja (Know Your Customer – KYC), kupunguza uwezekano wa udanganyifu wa utambulisho na kusaidia kufanya maamuzi bora zaidi katika utoaji wa mikopo.
Hatua hiyo pia inaweza kuchangia kujenga mazingira salama zaidi ya ukopeshaji, ambapo wakopaji waaminifu wanaweza kunufaika na upatikanaji wa huduma za fedha huku taasisi zikiongeza uwezo wa kudhibiti hatari zinazotokana na udanganyifu.

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
No comments:
Post a Comment