DAR ES SALAAM - Agosti 7, 2026: Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Bia, Kampuni ya Serengeti Breweries Limited (SBL) imeipa Tanzania sababu nyingine ya kujivunia baada ya bidhaa zake nne kutambuliwa kimataifa kwa ubora wa hali ya juu kupitia Tuzo za Gold Quality Awards 2026 zinazotolewa na taasisi maarufu duniani ya Monde Selection.
Katika mafanikio hayo, bia za Serengeti Lite, Serengeti Lager na Serengeti Lemon, pamoja na kinywaji kikali cha TZEE, zimetunukiwa tuzo hizo baada ya kuthibitishwa kukidhi viwango vya kimataifa vya ubora.
Tuzo za Gold Quality Awards hutolewa kwa bidhaa zinazofaulu mchakato wa kina wa tathmini unaofanywa na jopo huru la wataalamu wa kimataifa. Bidhaa hupimwa kwa kuzingatia vigezo mbalimbali, ikiwemo ubora wa jumla, ladha, mwonekano, ubunifu, taarifa kwa watumiaji na uzoefu wa matumizi, kabla ya kutambuliwa kuwa zimefikia viwango vinavyokubalika duniani.
Monde Selection ni taasisi huru ya kimataifa iliyoanzishwa mwaka 1961 mjini Brussels, Ubelgiji, na kwa zaidi ya miaka 65 imekuwa ikitathmini maelfu ya bidhaa kutoka sekta mbalimbali kama vile vyakula, bia, vinywaji vikali, bidhaa za afya na lishe pamoja na vipodozi. Kila mwaka, wataalamu zaidi ya 80 kutoka mataifa mbalimbali hushiriki katika mchakato huo wa tathmini, huku bidhaa kutoka takribani nchi 150 zikiwasilishwa kwa ajili ya kupimwa.
Mafanikio ya SBL yanaonesha matokeo ya uwekezaji wa muda mrefu katika teknolojia za kisasa za uzalishaji, mifumo madhubuti ya uhakiki wa ubora na ubunifu unaolenga kukidhi mahitaji ya watumiaji wa ndani na wa kimataifa.
Akizungumza kuhusu tuzo hizo, Mkurugenzi wa Ugavi wa Serengeti Breweries Limited, Joseph Cheloti, alisema kutambuliwa na Monde Selection ni ushahidi kuwa bidhaa za kampuni hiyo zinafikia viwango vya ubora vinavyotambulika duniani.
"Kupokea Tuzo za Gold Quality Awards kutoka Monde Selection ni heshima kubwa na uthibitisho kuwa bidhaa zetu zinakidhi viwango vya ubora vinavyotambulika kimataifa. Tunajivunia mafanikio haya ambayo yanadhihirisha kujitolea kwa wafanyakazi wetu, ubora wa malighafi tunazotumia pamoja na uimara wa mifumo yetu ya uzalishaji. Zaidi ya yote, tunawashukuru wateja wetu kwa kuendelea kutuamini na kutuunga mkono," alisema Cheloti.
Aliongeza kuwa kampuni itaendelea kuwekeza katika ubora, ubunifu na maendeleo ya bidhaa ili kuhakikisha watumiaji wa Tanzania na masoko mengine wanaendelea kupata vinywaji vinavyokidhi viwango vya juu vya kimataifa.
Kupokea Tuzo nne za Gold Quality Awards 2026 kwa wakati mmoja kunaimarisha zaidi hadhi ya Serengeti Breweries Limited kama mmoja wa wazalishaji wa vinywaji wenye viwango vya kimataifa, huku ikiendelea kuitangaza Tanzania kwenye ramani ya dunia kupitia ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini.
Kwa sekta ya viwanda na uzalishaji nchini, mafanikio haya yanathibitisha kuwa uwekezaji katika ubora, teknolojia na ubunifu unaweza kuiwezesha Tanzania kushindana na kushinda katika soko la kimataifa.
Endelea kufuatilia Kitomari Banking & Finance Blog kwa habari za uhakika kuhusu biashara, benki, uwekezaji, viwanda na maendeleo ya uchumi nchini Tanzania na duniani.

No comments:
Post a Comment