MWANZA - Agosti 30, 2026: Benki ya NMB imewataka wafanyabiashara wa mikoa ya Mwanza, Mara na Geita kutumia kikamilifu teknolojia za kifedha na akaunti rasmi za biashara ili kuongeza ufanisi, kufikia masoko mapya na kusimamia fedha zao kwa usahihi.
Wito huo umetolewa wakati wa NMB Business Executive Network, uliofanyika jijini Mwanza na kuwashirikisha wafanyabiashara pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya biashara.
Akizungumza katika jukwaa hilo, Mkuu wa Idara ya Biashara wa NMB, Deogratius Shirima, alisema mabadiliko ya teknolojia pamoja na kuongezeka kwa mahitaji ya wateja kunawalazimu wafanyabiashara kubadili namna wanavyopokea malipo na kuendesha shughuli zao za kila siku.
Alisema matumizi ya suluhisho za malipo ya kidijitali za NMB yanaweza kuwawezesha wafanyabiashara kurahisisha miamala, kuboresha usimamizi wa fedha na kuongeza uwezo wa biashara zao kushindana katika soko linalozidi kuwa la kidijitali.
Shirima pia alieleza kuwa NMB SME World Business Credit Card ni miongoni mwa suluhisho zinazolenga kurahisisha miamala ya biashara ndani na nje ya Tanzania, hivyo kuwawezesha wafanyabiashara kusimamia mahitaji mbalimbali ya kifedha kwa ufanisi zaidi.
Aidha, alisema NMB imeendelea kuboresha huduma zake za Bank Guarantee, ambapo dhamana za zabuni zisizohitaji dhamana ya mali (Unsecured Bid Bonds) zinaweza kufikia hadi Dola za Marekani milioni 10, hatua inayolenga kuwawezesha wafanyabiashara kushiriki katika fursa kubwa zaidi za zabuni na mikataba.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Biashara kwa Wateja Wadogo na wa Kati (SME) wa NMB, Leah Mwakang’ata, aliwahimiza wafanyabiashara kutenganisha fedha binafsi na fedha za biashara kwa kutumia akaunti rasmi za biashara.
Alisema utaratibu huo unawasaidia wafanyabiashara kufuatilia mapato na matumizi ya biashara kwa usahihi, kujenga historia nzuri ya kifedha na hatimaye kupata huduma za kifedha zinazolingana na mahitaji na ukubwa wa biashara zao.
“Kutenganisha fedha binafsi na fedha za biashara ni hatua muhimu katika kujenga biashara yenye msingi mzuri wa kifedha.” alisema Mwakang’ata.
Naye Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Mwanza, Gabriel Mugini, alisema mazingira ya biashara mkoani Mwanza yanaendelea kuvutia wawekezaji kutokana na fursa mbalimbali zilizopo.
Mugini aliwataka wafanyabiashara kutumia ipasavyo fursa za kifedha na kiteknolojia zinazopatikana ili kukuza na kupanua shughuli zao, kuongeza ushindani na kuchangia zaidi katika maendeleo ya uchumi wa Mkoa wa Mwanza na Tanzania kwa ujumla.
Jukwaa la NMB Business Executive Network ni sehemu ya jitihada za NMB za kuwakutanisha wafanyabiashara na wadau mbalimbali kwa ajili ya kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto na kutafuta suluhisho zinazoweza kusaidia kukuza biashara.
Endelea kufuatilia Kitomari Banking & Finance Blog kwa habari, uchambuzi na taarifa mbalimbali kuhusu biashara, benki na sekta ya fedha Tanzania.







No comments:
Post a Comment