Foreign Exchange Rates

Absa Loan Campaign_160426

Absa Loan Campaign_160426

CRDB Bank Advert_070325

Thursday, 2 July 2026

KADI MPYA YA NMB YAFUNGUA FURSA ZA MITAJI KWA WAFANYABIASHARA WADOGO NA WA KATI

Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi (katikati), Mkurugenzi wa Mastercard anayesimamia biashara Afrika Mashariki, Imelda Ngunzu, na Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini, Baraka Ladislaus, wakizindua rasmi kadi maalumu ya NMB SME World Business Credit Card jijini Arusha.

ARUSHA – Benki ya NMB, kwa kushirikiana na Mastercard, imezindua NMB SME World Business Credit Card, bidhaa mpya ya kifedha inayolenga kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs) kupata mtaji wa haraka, kufanya malipo ya ndani na kimataifa kwa urahisi, na kuendesha biashara zao kwa ufanisi zaidi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika jijini Arusha, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, alisema kadi hiyo imebuniwa kukidhi mahitaji ya wafanyabiashara wanaohitaji mtaji wa muda mfupi ili kuendeleza shughuli zao za kila siku.

Alieleza kuwa kadi hiyo inatoa mkopo wa hadi Shilingi milioni 50, kulingana na uwezo wa kifedha wa mteja, pamoja na kipindi cha hadi siku 53 bila riba, endapo deni litarejeshwa ndani ya muda huo. Mfumo huo unawapa wafanyabiashara nafasi ya kuongeza bidhaa, kulipa wasambazaji kwa wakati na kushughulikia changamoto za mtaji bila kuathiri mzunguko wa biashara zao.

Mbali na huduma ya mkopo, NMB SME World Business Credit Card inaweza kutumika kupitia mtandao wa Mastercard katika mamilioni ya maeneo duniani, hivyo kuwawezesha wafanyabiashara kufanya malipo ya kimataifa kwa usalama na urahisi.

Kadi hiyo pia inakuja na manufaa mbalimbali yanayoongeza thamani kwa watumiaji wake, ikiwemo bima ya matibabu ya safari yenye thamani ya hadi Dola za Marekani 100,000, bima ya mizigo, huduma za VIP Lounge katika zaidi ya viwanja vya ndege 400 duniani, pamoja na punguzo maalumu katika hoteli na huduma nyingine mbalimbali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mastercard anayesimamia biashara za SMEs Afrika Mashariki na Visiwa vya Bahari ya Hindi, Imelda Ngunzu, alisema uzinduzi wa kadi hiyo unaonesha dhamira ya Mastercard na NMB ya kusaidia ukuaji wa biashara ndogo na za kati kupitia suluhisho za kisasa za kifedha.

Alisema upatikanaji wa mtaji kwa wakati pamoja na mfumo salama wa kufanya malipo ni miongoni mwa mambo muhimu yatakayowawezesha wafanyabiashara kuongeza ushindani na kupanua shughuli zao katika soko la ndani na la kimataifa.

Sambamba na uzinduzi huo, NMB ilisisitiza kuwa itaendelea kuwekeza katika teknolojia za malipo ya kidijitali ikiwemo huduma za QRPayByLink na mashine za POS, hatua inayolenga kuboresha ukusanyaji wa mapato, kuongeza ufanisi wa biashara na kuunga mkono jitihada za Tanzania kuelekea uchumi jumuishi wa kidijitali.

Uzinduzi wa NMB SME World Business Credit Card unathibitisha dhamira ya benki hiyo ya kuendelea kutoa suluhisho bunifu za kifedha zinazowawezesha wafanyabiashara kukua, kuongeza ukwasi na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Tanzania.




No comments:

Post a Comment