Foreign Exchange Rates

Equity Bank Advert_12 February 2026

CRDB Bank Advert_070325

Global Sanctions Compliance Masterclass

Saturday, 7 March 2026

WAZIRI WA FEDHA BALOZI KHAMIS MUSSA OMAR AONGOZA WATEJA WA NBC KATIKA FUTARI MAALUM

Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar (katikati) akipokea zawadi maalum kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NBC, Dk. Elirehema Doriye (kushoto), wakati wa hafla ya futari iliyoandaliwa na benki hiyo kwa ajili ya wateja wake jijini Dar es Salaam. Anayeshuhudia ni Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Bw. Theobald Sabi (kulia).
Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar (mbele) akiwaongoza wageni waalikwa kupata futari wakati wa hafla ya futari iliyoandaliwa na Benki ya NBC kwa ajili ya wateja wake jijini Dar es Salaam.

Azikumbusha Taasisi za Fedha Kusaidia Kutimiza Dira ya Taifa 2050

Dar es Salaam, Machi 6, 2026 — Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, aliwaongoza baadhi ya Waislamu jijini Dar es Salaam kushiriki hafla ya futari iliyoandaliwa na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa ajili ya wateja na wadau mbalimbali wa benki hiyo.

Hafla hiyo iliyofanyika katika Hoteli ya Johari Rotana, Dar es Salaam, ililenga kuimarisha mahusiano kati ya benki hiyo na wadau wake, huku ikitumika pia kama jukwaa la kukumbushana wajibu wa taasisi za fedha katika kuchangia maendeleo ya taifa.

Katika hotuba yake, Waziri Omar alizikumbusha taasisi za fedha nchini umuhimu wa kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, inayolenga kujenga Tanzania yenye uchumi wa kisasa unaochochewa na uwekezaji, viwanda, biashara pamoja na ubunifu wa kidijitali.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, viongozi wa dini pamoja na wateja na wadau wa benki hiyo. Uongozi wa NBC uliwakilishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Dk. Elirehema Doriye, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Theobald Sabi, na maofisa wengine waandamizi.

Taasisi za Fedha Zasisitizwa Kujenga Uaminifu

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Omar aliishukuru na kuipongeza NBC kwa kuandaa tukio hilo la kiimani, akisisitiza kuwa uthabiti wa sekta ya fedha ni nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa taifa.

Alieleza kuwa ili kufanikisha hilo, ni muhimu taasisi za fedha kuendelea kujenga uaminifu mkubwa kwa wateja wao.

Hii ndiyo sababu tunazithamini sana taasisi za fedha zinazojenga ukaribu zaidi na wateja pamoja na wadau wake muhimu. Tunaamini kwamba uaminifu ndio msingi wa mzunguko wa fedha katika uchumi, kama ilivyo kaulimbiu yenu ya ‘Daima Karibu Nawe’. Nawapongeza sana NBC kwa kuendeleza utamaduni huu,” alisema.

Aidha, alibainisha kuwa Serikali imeweka msisitizo mkubwa katika kujenga uchumi jumuishi, shindani na unaotegemea uzalishaji wa ndani, hivyo sekta ya fedha ina nafasi kubwa katika kufanikisha azma hiyo.

Ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, sekta ya fedha hasa benki zina jukumu la msingi — si tu kutoa huduma za kifedha bali pia kuwa wawezeshaji wa mageuzi makubwa ya kiuchumi,” alisisitiza.

Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa taasisi za fedha ili ziweze kutoa mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya uchumi wa nchi.

NBC Yaahidi Kuimarisha Ushirikiano na Wadau

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NBC, Dk. Elirehema Doriye, alisema benki hiyo itaendelea kuendeleza utamaduni wa kuandaa matukio kama hayo kwa ajili ya kuimarisha mahusiano na wadau wake muhimu.

Alisisitiza kuwa mafanikio ya NBC yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na ushirikiano mzuri uliopo kati ya benki hiyo, Serikali na wateja wake.

Tunatambua pia nafasi ya Mwenyezi Mungu katika kutuwezesha kuendesha taasisi zinazogusa ustawi wa maisha ya watu. Ndiyo maana tumekuwa tukitoa wito kwa wananchi kuwaombea viongozi wetu wa kitaifa ili waendelee kuongoza kwa weledi na ufanisi,” alisema.

NBC Yaendelea Kupanua Huduma za Kifedha Zinazozingatia Misingi ya Kiislamu

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Bw. Theobald Sabi, alitumia fursa hiyo kuwashukuru wadau wa benki hiyo kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa, akiwemo Serikali, viongozi wa dini na wateja mbalimbali.

Alieleza kuwa kupitia ushirikiano huo, NBC imefanikiwa kubuni na kutoa huduma mbalimbali za kifedha zinazozingatia misingi ya Kiislamu.

Huduma hizo ni pamoja na akaunti za akiba na biashara, akaunti za uwekezaji wa muda maalum (Fixed Investment Accounts), pamoja na huduma za uwezeshaji wa kifedha kupitia mfumo wa Murabaha. Pia alitaja huduma ya Rariba, inayolenga kuwawezesha wafanyabiashara wadogo pamoja na kutoa suluhisho la kifedha kwa wateja binafsi na wa kibiashara.

Kwa mujibu wa Sabi, zaidi ya wateja 43,000 wanahudumiwa kupitia dirisha hilo la huduma za kifedha zinazozingatia misingi ya Kiislamu, wakiwa na amana zinazozidi Shilingi bilioni 80, huku uwezeshaji wa kifedha uliotolewa kupitia dirisha hilo ukizidi Shilingi bilioni 46.

Tunawahamasisha wateja na wadau wengi zaidi kuendelea kutumia huduma hizi,” alisema.

Aidha, alitoa shukrani kwa Serikali kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki kwa ukuaji wa sekta ya fedha na biashara nchini. Pia aliipongeza Wizara ya Fedha pamoja na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kwa usimamizi thabiti wa sekta ya fedha uliosaidia kuimarisha mifumo ya kifedha nchini.

Sabi alisisitiza kuwa NBC itaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine katika kuwezesha sekta ya fedha kuchochea uzalishaji, kusaidia biashara ndogo, za kati na kubwa, na kuongeza ujumuishi wa kifedha kupitia mifumo ya kidijitali pamoja na huduma zinazozingatia imani za kidini. 







No comments:

Post a Comment