Mbeya, Tanzania – Benki ya NMB imesema kuwa kwa sasa ina uwezo wa kumkopesha mteja mmoja zaidi ya Sh bilioni 500 kwa ajili ya uendeshaji wa biashara na shughuli nyingine za uzalishaji ikiwemo kilimo, mifugo, viwanda na uchimbaji wa madini, kutokana na mtaji wake mkubwa.
Mkuu wa Idara ya Biashara wa NMB, Alex Mgeni, aliyasema hayo jijini Mbeya wakati wa chakula cha jioni na wafanyabiashara wa Kanda ya Nyanda za Juu ambao ni wateja wakubwa wa benki hiyo.
Mgeni alisema lengo la mikopo hiyo ni kukuza shughuli za wateja, huku ikitolewa kupitia masuluhisho mbalimbali ambayo benki imeyaandaa kulingana na mahitaji ya kila mteja. Pia aliwahimiza wateja kuendelea kutumia huduma za kidijitali ikiwemo NMB Mkononi na Internet Banking.
“Huduma hizi zinalenga kumpunguzia mteja muda na gharama za kufika kwenye matawi yetu,” alisema Mgeni.
Aliongeza kuwa NMB imeanzisha pia mkopo maalumu wa nishati safi ya kupikia kwa wafanyabiashara, wenye riba ya 1% kwa mwezi au 12% kwa mwaka.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Kilimo wa NMB, Nsolo Mlozi, alisema sehemu kubwa ya wateja wa NMB Kanda ya Nyanda za Juu wanajihusisha na mnyororo wa thamani wa kilimo, ambapo wengi wanakopa kwa ajili ya mitambo ya kilimo, magari ya kusafirisha mazao, ununuzi wa mazao na pembejeo.
Alibainisha kuwa baadhi ya mazao ya chakula kama viazi na mpunga yameanza kubadilika na kuwa ya kibiashara kutokana na uzalishaji kuongezeka.
“Tunatarajia pia kuanza kutoa mikopo ya vifaa vya umwagiliaji ili kuongeza tija ya kilimo na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi,” alisema Mlozi.
Meneja wa NMB Kanda ya Nyanda za Juu, Wogofya Mfalamagoha, alisema NMB ndiyo benki kubwa zaidi nchini, ikiwa na matawi katika kila wilaya na mtandao mpana wa mawakala hadi vijijini.
Mfalamagoha alifafanua kuwa miaka miwili iliyopita NMB ilikuwa na mawakala 20,000 pekee, lakini sasa imefikia 60,000 kote nchini, hivyo akawahimiza wananchi kuendelea kuamini na kutumia huduma za benki hiyo.
Baadhi ya wateja walioshiriki hafla hiyo waliipongeza NMB kwa mchango mkubwa katika kukuza biashara zao na maendeleo ya kiuchumi.
Mhandisi Ralph Makundi, mmoja wa wateja, alisema mikopo kutoka NMB imemsaidia kupata kandarasi kubwa na kukuza kampuni yake ya ujenzi.
“Nilipoanza kukopa, kampuni yangu ilikuwa ya daraja la sita, lakini sasa imefika daraja la kwanzakutokana na msaada wa NMB,” alisema Makundi.


No comments:
Post a Comment