Dar es Salaam, Septemba 22, 2025 – Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imetoa elimu maalum kwa wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika Kusini kuhusu masoko ya fedha za kigeni pamoja na muelekeo wa hali ya kiuchumi nchini Tanzania. Hatua hiyo inalenga kuwajengea uwezo na ufanisi zaidi wafanyabiashara hao ili waweze kufanya maamuzi sahihi katika ununuzi wa fedha za kigeni na uwekezaji.
Akizungumza kwenye Mkutano wa Jukwaa la Wafanyabiashara wa Afrika Kusini nchini Tanzania (SABF) uliofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya Masoko ya Fedha za Kigeni wa NBC, Bi. Juliana Mwapachu, alisema uelewa mpana wa masoko ya fedha za kigeni unaweza kuwasaidia wafanyabiashara kuepuka hasara zinazojitokeza kutokana na mabadiliko ya thamani ya fedha.
“Huu ni mwendelezo wa jitihada za NBC kama benki kinara katika kuwahudumia wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika Kusini. Tumekuwa tukiwaletea mada mbalimbali za kiuchumi na kibiashara ili kuwajengea uelewa unaosaidia biashara zao kuendeshwa kwa njia rafiki kwa taasisi za kifedha na mamlaka husika, na kuepuka changamoto zinazoweza kuwakwamisha,” alisema Bi. Mwapachu.
Katika mada yake, alieleza mwenendo wa uchumi wa Tanzania kwa mwaka 2025 na matarajio ya mwaka 2026, akisisitiza kuwa elimu ya kutosha kuhusu masoko ya fedha itawawezesha wafanyabiashara kufanya maamuzi bora juu ya muda na njia ya kununua au kubadilisha fedha za kigeni kwa viwango rafiki.
Aliongeza kuwa, mbali na huduma za fedha za kigeni, NBC imejipanga kuendelea kutoa huduma za ushauri wa kitaalamu kwa wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao nje ya Tanzania, hususan Afrika Kusini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa SABF, Bw. Manish Thakrar, alisema elimu hiyo ni muhimu sana kwa wafanyabiashara ambao mara kwa mara hununua fedha za kigeni kwa ajili ya kuagiza bidhaa kutoka nje.
“Elimu hii imekuja kwa wakati muafaka, hasa kipindi hiki ambapo thamani ya Dola ya Kimarekani imeshuka kwa karibu Sh200. Sasa wafanyabiashara wanaweza kuona huu kama muda sahihi wa kuagiza na kuuza bidhaa nje ya nchi, jambo litakaloongeza kasi ya biashara na kukuza uchumi wetu,” alisema Bw. Thakrar.
Aliongeza kutoa wito kwa Serikali kuhakikisha inaendelea kusimamia mikakati madhubuti ya kuimarisha thamani ya Shilingi ya Kitanzania dhidi ya sarafu za kigeni, hususan Dola ya Kimarekani, ili kuchochea ustawi wa biashara na kupunguza gharama za bidhaa kutoka nje ya nchi.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wanachama wa SABF, wawakilishi wa taasisi mbalimbali, maafisa wa ubalozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania pamoja na maafisa kutoka benki ya NBC, ambayo ilikuwa mdhamini mkuu wa tukio hilo.










No comments:
Post a Comment