Foreign Exchange Rates

CRDB Bank Advert_070325

Selcom Pesa Advert_110225

Selcom Pesa Advert_110225

Standard Chartered Advert_300125

Standard Chartered Advert_300125

Monday, 4 August 2025

NMB YAWEKA MSISITIZO KATIKA KUTOA ELIMU NA MIKOPO NAFUU KATIKA MAONESHO YA NANE NANE

Dodoma, 2 Agosti 2025 – Mkuu wa Kitengo cha Biashara Serikalini kutoka Benki ya NMB, makao makuu, Vicky Bishubo, amesema benki hiyo imepanga kutumia maonesho ya wakulima ya Nane Nane kutoa elimu kwa wananchi kuhusu fursa zinazotolewa na benki hiyo katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi nchini.

Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa maonesho ya wakulima kitaifa katika viwanja vya Nzuguni, Dodoma—uliofanywa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango—Bishubo alisema Benki ya NMB imejidhatiti kupanua wigo wa huduma kwa wadau wa sekta hizo kwa kuwapatia mikopo yenye riba nafuu, ili kuongeza tija katika shughuli zao za kiuchumi.

“Mheshimiwa Makamu wa Rais, naomba nitumie nafasi hii kukushukuru na kukupongeza wewe binafsi pamoja na Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi katika sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji,” alisema Bishubo.

Alisema dhamira ya NMB ni kuongeza thamani na faida katika shughuli za kilimo, hatua itakayochangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi na kuongeza mchango kwenye Pato la Taifa.

Bishubo pia aliwapongeza washiriki wote wa maonesho—wakulima, wafugaji, wavuvi, na wananchi kwa ujumla—kwa muitikio mkubwa waliouonesha, akisisitiza kuwa maonesho hayo ni jukwaa muhimu kwa kubadilishana maarifa na kuonyesha fursa zilizopo katika sekta ya kilimo.

“Na sisi Benki ya NMB tunawathibitishia kuwa tuko pamoja nao kuhakikisha wanasonga mbele zaidi,” aliongeza.

NMB YADHAMINI MAONESHO YA NANENANE KWA KISHINDO

Bishubo alisema kuwa Benki ya NMB inajivunia kuwa mmoja wa wadhamini wakuu wa Maonesho ya Nane Nane mwaka huu, ambapo imetoa mchango wa shilingi milioni 100 kusaidia maandalizi na ufanikishaji wa maonesho hayo.

“Tunaamini kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yetu, na tumejitolea kwa dhati kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha sekta hii muhimu,” alisema.

Kwa kutambua kuwa kilimo cha kisasa kinahitaji uwekezaji katika miundombinu, benki hiyo imekuwa ikishiriki maonesho ya Nane Nane katika kanda zote nchini, ikiwa na mikakati kabambe ya kuwawezesha wakulima, wafugaji, na wavuvi, hasa wanaojishughulisha na mazao ya biashara kama kahawa, tumbaku, korosho, ufuta na mengineyo.

“Ndani ya miaka mitano pekee, tumefungua zaidi ya akaunti milioni moja kwa ajili ya wakulima, wafugaji, na wavuvi kote nchini,” alibainisha.

MIKOPO NA BIMA KWA KASI MPYA

Vicky Bishubo alisema kuwa hadi sasa, zaidi ya shilingi bilioni 100 zimelenga mikopo kwa wafugaji, ikiwa ni pamoja na kununua na kunenepesha mifugo, kujenga miundombinu ya maji, na kuwekeza katika mifugo ya kisasa.

Kwa upande wa mazao ya kilimo, NMB imetoa mikopo ya:

  • Shilingi bilioni 182 kwa wakulima wa kahawa
  • Shilingi bilioni 499 kwa tumbaku
  • Shilingi bilioni 175 kwa sukari
  • Shilingi bilioni 131 kwa zao la pamba

Benki hiyo pia imeendeleza huduma ya MshikoFasta, ambapo mkulima kupitia NMB Mkononi anaweza kupata mkopo wa hadi shilingi 1,000,000 papo hapo bila dhamana, kwa ajili ya shughuli za kilimo.

Aidha, NMB inatoa bima mbalimbali kwa wakulima, ikiwa ni pamoja na:

  • Bima ya hali ya hewa
  • Bima ya mazao shambani
  • Bima ya moto na wizi kwa mazao yaliyohifadhiwa
  • Bima ya vifaa vya kilimo
  • Bima ya mifugo

“Niwaombe wateja wetu na Watanzania kwa ujumla kufika kwenye tawi lolote la NMB kupata huduma hizi muhimu,” alihitimisha.


Endelea kufuatilia Kitomari Banking & Finance Blog kwa taarifa zaidi kuhusu mchango wa taasisi za kifedha katika kukuza uchumi wa kilimo, mifugo na uvuvi nchini Tanzania.









No comments:

Post a Comment