DAR ES SALAAM – Airtel Money kwa kushirikiana na Benki ya I&M wamezindua rasmi mpango maalum unaolenga kuwawezesha wanawake wajasiriamali nchini kupitia elimu ya kifedha na nyenzo muhimu za kukuza biashara, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha maisha ya wanawake na kuchochea usawa wa kijinsia.
Mpango huu ni sehemu ya Mkakati wa Uendelevu wa Benki ya I&M Tanzania unaojikita kwenye nguzo kuu tatu: ujumuishaji wa kifedha, elimu ya kifedha, na uwajibikaji wa mazingira. Mkakati huu unaendana na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs), hasa SDG 5 (Usawa wa Kijinsia) na SDG 13 (Hatua dhidi ya Mabadiliko ya Tabianchi).
Kupitia huduma ya Kamilisha, iliyoundwa kwa pamoja na Airtel Money na Benki ya I&M, wateja hupata mikopo midogo kupitia simu zao za mkononi, hata wanapokosa salio kwenye akaunti zao za Airtel Money, ili waweze kutuma pesa au kulipa bili muhimu.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Bw. Charles Kamoto, alisema:
"Kuna matumizi makubwa ya Airtel Money nchini, na tunalenga kujenga uwezo wa kifedha hasa kwa wanawake, kwa kuwawezesha kutumia huduma za kifedha za kidijitali kwa ufanisi. Tunataka kuhakikisha kuwa wateja wetu wana ujasiri na ujuzi wa kutumia teknolojia hii kwa maendeleo yao."
Kamoto alibainisha kuwa zaidi ya asilimia 65 ya watu wazima nchini bado hawajafikiwa na huduma rasmi za kifedha, huku wanawake wakiwa kwenye mazingira magumu zaidi.
"Kupitia mpango huu, tunapunguza pengo la elimu ya kifedha. Kwa kuwa chini ya asilimia 30 ya wanawake wanamiliki simu janja, tumejumuisha mafunzo ya moja kwa moja ili kuwajengea uelewa wa matumizi ya programu za kifedha."
Katika mafunzo ya siku moja yaliyofanyika jijini Dar es Salaam kama sehemu ya uzinduzi, wanawake zaidi ya 50 walihudhuria warsha shirikishi kuhusu usimamizi wa fedha, matumizi ya fedha kidijitali, na mbinu endelevu za biashara — yakilenga kuimarisha uwezo wao wa kiuchumi huku yakizingatia mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa I&M Bank Tanzania, Bw. Zahid Mustafa, alisema:
"Hii ni sehemu ya dhamira yetu ya kuifanya benki kuwa jukwaa la kuleta mabadiliko chanya. Tunajivunia kushirikiana na Airtel katika mpango huu, ambapo tulianza kwa kutoa mafunzo kwa wanawake 60 kwa udhamini kamili. Mtaala wa mafunzo haya umetayarishwa kwa kushirikiana na Grant Thornton na utaendelea kuboreshwa kwa kuzingatia mrejesho kutoka kwa washiriki."
Licha ya ukuaji wa huduma za fedha kidijitali nchini, biashara nyingi ndogondogo zinazoongozwa na wanawake bado hazijafikiwa na huduma rasmi za kifedha kutokana na ukosefu wa elimu na zana za kifedha. Mpango huu unalenga kuziba pengo hilo kwa kuimarisha ujuzi wa vitendo na kuongeza ujasiri kwa wanawake kuingia katika mfumo rasmi wa kifedha.
Tangu kuanzishwa kwa huduma ya Kamilisha, zaidi ya TZS bilioni 392 zimetolewa kama mikopo, ambapo asilimia 46ya mikopo hiyo imewafikia wanawake. Hadi sasa, zaidi ya Watanzania milioni tano wameingia kwenye mfumo rasmi wa kifedha kupitia huduma hii.
Kama sehemu ya mpango huu, Benki ya I&M imeahidi kupanda mti mmoja kwa kila wanawake 100 watakaopata mkopo, ikiwa na lengo la kupanda miti 8,000 kila mwaka. Mpango huu wa kimazingira unatekelezwa kwa ushirikiano na taasisi ya Africa Transformation Initiative (ATI) ambayo itasimamia upatikanaji, upandaji, na ufuatiliaji wa miti hiyo nchini kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.
No comments:
Post a Comment