DAR ES SALAAM, TANZANIA – 30 JULAI 2025 – Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye matumizi makubwa ya pombe haramu barani Afrika, jambo ambalo linaelezwa kuwa tishio kubwa kwa afya ya umma, huku pia likiathiri mapato ya serikali na ukuaji wa sekta rasmi ya biashara ya vinywaji.
Taarifa hii imebainishwa leo jijini Dar es Salaam katika mkutano wa wadau wa sekta ya pombe, uliowakutanisha wawakilishi kutoka Serikalini, sekta binafsi na taasisi za udhibiti, kujadili njia bora za kukabiliana na changamoto hiyo. Mkutano huo ulifanyika chini ya kaulimbiu: "Kuungana Kupambana na Pombe Haramu Nchini Tanzania."
Kwa mujibu wa takwimu zilizojadiliwa katika mkutano huo, asilimia 55 ya pombe inayotumika nchini inakadiriwa kuwa haramu – ikiwemo pombe ya kienyeji isiyosajiliwa, ya magendo, na ile inayouzwa bila kulipa kodi au kukaguliwa kwa viwango vya ubora.
“Pombe haramu bado ni suala tete nchini Tanzania. Inahatarisha maisha ya watu kutokana na kutotimiza viwango vya usalama wa kiafya, huku pia ikipunguza mapato ya serikali na kushusha ushindani kwa biashara halali,” alisema Hussein Sufian, Mwenyekiti wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI).
Mkutano huo uliambatana na uzinduzi wa utafiti wa kitaifa kuhusu pombe haramu, ambao utafanyika kwa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi ili kuchunguza sababu, ukubwa, na athari za biashara ya pombe isiyo halali nchini.
WAZALISHAJI WATOA MAONI
Akizungumza kwa niaba ya wazalishaji wa bia nchini, Mkurugenzi Mtendaji wa Serengeti Breweries Limited (SBL), Obinna Anyalebechi, alisema sekta ya pombe iko tayari kutumia matokeo ya utafiti huo kukuza bidhaa halali zitakazovutia watumiaji wa pombe haramu kuhamia bidhaa zilizosajiliwa.
“Tunataka kutumia ushahidi huu kubuni bidhaa bora, nafuu na salama ili kuwavuta walaji kutoka sokoni mwa pombe haramu kwenda kwenye bidhaa halali,” alisema Anyalebechi.
SERIKALI YAAHIDI KUCHUKUA HATUA ZA KISERA
Kwa upande wa Serikali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alieleza kuwa serikali imejipanga kutumia matokeo ya utafiti huo kuunda sera na hatua za kudhibiti pombe haramu nchini.
“Mkutano huu ni hatua muhimu katika kuratibu juhudi zetu za kupambana na biashara ya pombe haramu. Tunahitaji suluhisho la pamoja, la muda mrefu, linalotegemea takwimu na manufaa ya Watanzania,” alisema Chalamila.
KUHUSU SBL
Ilianzishwa mwaka 1988 kama Associated Breweries, Serengeti Breweries Limited (SBL) ni kampuni ya pili kwa ukubwa wa uzalishaji wa bia nchini Tanzania. Ikiwa chini ya EABL/Diageo tangu 2010, kampuni imewekeza katika viwango vya juu vya ubora wa kimataifa na imekuwa ikitoa fursa nyingi za ajira kwa Watanzania.
SBL huzalisha chapa mbalimbali za bia kama Serengeti Premium Lager, Serengeti Lite, Serengeti Lemon, Pilsner Lager, Kibo Gold, Guinness Stout, Guinness Smooth, na Senator. Pia, huchakata vileo maarufu vya kimataifa kama Johnnie Walker, Smirnoff Vodka, Baileys, na nyinginezo.
MAWASILIANO ZAIDI:
Rispa Hatibu
Meneja Mawasiliano na Uendelevu, SBL
📞 Simu: +255 685 260 901
📧 Barua pepe: Rispa.Hatibu@diageo.com
Fuatilia Blogu Yetu kwa Taarifa Zaidi
Kwa uchambuzi wa kina kuhusu masuala ya viwanda, biashara, sera, na maendeleo ya sekta binafsi nchini, endelea kufuatilia Kitomari Banking & Finance Blog – blogu yako ya kuaminika kwa habari makini za kiuchumi na kifedha.









No comments:
Post a Comment