DAR ES SALAAM: Katika kuadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwake nchini Tanzania, Vodacom Tanzania PLC imezindua kampeni maalum ya kitaifa inayojulikana kama “Tupo Nawe, Tena na Tena”. Kampeni hii ya miezi minne inalenga kuonyesha mchango wa Vodacom katika maisha ya kila siku ya Watanzania, hasa katika zama hizi za mabadiliko ya kidijitali.
Kwa robo karne sasa, Vodacom imekuwa nguzo muhimu katika kuwaunganisha Watanzania kupitia teknolojia mbalimbali. Kampuni hiyo imepitia hatua mbalimbali – kutoka huduma za msingi za mawasiliano hadi kuwa kinara katika huduma za kisasa kama vile 5G, M-Pesa, afya mtandaoni, na elimu kwa njia ya simu.
Kupitia kampeni hii, Vodacom inatoa shukrani za dhati kwa wateja wake, wakisisitiza kuwa mafanikio yao yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na uaminifu na ushirikiano wa Watanzania kwa miaka yote 25.
“Tumeendelea kubadilika na kuwekeza katika ubunifu ili kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na huduma bora, za kisasa na zinazoendana na mahitaji ya wakati huu,” imeeleza kampuni hiyo kupitia taarifa rasmi.
Kwa miaka mingi, Vodacom imewekeza katika kukuza uchumi wa kidijitali nchini kwa kushirikiana na serikali, taasisi za kifedha, na sekta binafsi, lengo likiwa ni kuendeleza ushirikishwaji wa kijamii na kiuchumi.
Katika miaka ijayo, kampuni hiyo imeahidi kuendelea kuwa msukumo wa mabadiliko ya kidijitali nchini, ikilenga kujenga jamii jumuishi na yenye fursa sawa za maendeleo kupitia teknolojia.







No comments:
Post a Comment