Tanga, Tanzania – 4 Julai 2025
Ili kuhamasisha elimu ya kifedha na kuongeza uelewa wa bima miongoni mwa Watanzania, Stanbic Bank Tanzania kwa kushirikiana na Alliance Life Insurance na Jubilee Allianz Insurance, waliandaa kliniki ya bure ya elimu ya bima mbele ya tawi la benki hiyo jijini Tanga.
Katika kliniki hiyo, wakazi wa Tanga walipata fursa ya kuzungumza ana kwa ana na wataalamu wa sekta ya bima na benki, kuhusu huduma mbalimbali kama bima ya maisha, afya na mali, wakifundishwa namna ya kutumia bima kulinda maisha na rasilimali zao.
“Bima mara nyingi huonekana kama ya watu wachache, lakini ni msingi wa usalama wa maisha ya muda mrefu,” alisema Jumanne Mbepo, Meneja Mwandamizi wa Bima wa Stanbic Bank Tanzania.
Stanbic Bank inaendesha pia vipindi vya mtandaoni vya elimu ya bima, ili kuwafikia wananchi wengi zaidi kote nchini kwa njia rahisi na ya kidijitali.
Wakazi wengi wa Tanga walifurahishwa na tukio hilo. Kennedy Wanga, mmoja wa washiriki, alisema:
“Nilidhani bima ni kwa watu wenye fedha tu. Leo nimeelewa kuwa hata mimi naweza kujilinda na kusaidia familia yangu.”
Tukio hili ni sehemu ya jitihada za Stanbic Bank za kuimarisha ujumuishaji wa kifedha, na kuonesha dhamira yake ya kuchochea maendeleo endelevu kwa kauli mbiu:
“Tanzania ni nyumbani kwetu, tunachochea maendeleo yake.”
No comments:
Post a Comment