Zanzibar, 26 Februari 2025 – Vodacom Tanzania PLC imetia saini ushirikiano wa kimkakati na Shirika la Miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Zanzibar (ZICTIA) ili kuboresha huduma za mawasiliano na kuharakisha mabadiliko ya kidijitali visiwani Zanzibar. Mkataba huu, uliosainiwa katika ofisi za Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, unairuhusu Vodacom kutumia miundombinu ya nyaya za chini ya bahari inayomilikiwa na serikali, hatua itakayoboresha uwezo wa mawasiliano ya sauti na data katika visiwa hivyo.
Mkurugenzi wa Mtandao wa Vodacom, Andrew Lupembe, alieleza dhamira ya kampuni katika kuimarisha mawasiliano Zanzibar. “Kama kampuni inayoongoza katika teknolojia, tunaelewa kuwa mawasiliano ni msingi wa ukuaji wa uchumi na ubunifu. Kupitia ushirikiano huu na ZICTIA, tunahakikisha kuwa biashara, taasisi, na wananchi wa Zanzibar wanaweza kuwasiliana, kupata huduma za kidijitali, na kufanya miamala bila usumbufu.”
Ushirikiano huu ni hatua muhimu katika mageuzi ya kidijitali Zanzibar, ukiweka visiwa hivi katika nafasi bora kama kitovu cha mawasiliano na ubunifu. Kwa kuunganishwa kwa miundombinu ya Vodacom na mfumo madhubuti wa TEHAMA wa ZICTIA, Zanzibar itanufaika na mfumo wa kisasa wa mawasiliano wa kasi ya juu.
No comments:
Post a Comment