Foreign Exchange Rates

Selcom Pesa Advert_110225

Selcom Pesa Advert_110225

Standard Chartered Advert_300125

Standard Chartered Advert_300125

DStv Advert_090724

DStv Advert_090724

Tuesday, 18 February 2025

WAZIRI MKUU ATOA WITO UWEKEZAJI WA BENKI YA NMB KATIKA ELIMU UIGWE


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa taasisi za umma na binafsi kuiga mfano wa Benki ya NMB katika kuwekeza kwenye sekta ya elimu, akieleza kuwa ufadhili huo una faida kubwa kwa maendeleo ya taifa.


Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam alipotembelea banda la NMB katika Maadhimisho ya Miaka 20 ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC).


Wakati wa ziara hiyo, Waziri Mkuu alipokea maelezo kutoka kwa Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Bw Juma Kimori, kuhusu jinsi benki hiyo ilivyo mstari wa mbele katika kuboresha upatikanaji wa elimu ya juu kwa kuwekeza zaidi ya TZS bilioni 200 kwenye mikopo nafuu.


“Mchango wa NMB katika sekta ya elimu ni mkubwa na wa kuigwa. Nawashukuru kwa juhudi zenu za kuunga mkono sera za serikali za kuboresha elimu kupitia mikopo na ufadhili wa wanafunzi wasiokuwa na uwezo,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.


Bw Kimori alieleza kuwa NMB kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, inatoa mikopo ya elimu ya juu kwa riba ya 9%, lengo likiwa ni kuwasaidia wazazi na walezi kulipia ada za watoto wao au kujiendeleza kielimu wao wenyewe.


“Lengo letu ni kupunguza changamoto za kifedha kwa wanafunzi wa elimu ya juu na vyuo vya ufundi,” alisema Bw Kimori.

Kwa wanafunzi wanaohitaji msaada wa haraka wa kifedha, kiongozi huyo alisema NMB ina huduma ya Mshiko Fasta, inayotoa mikopo ya TZS 1,000 hadi TZS milioni 1 bila dhamana au kufika katika tawi lolote la benki hiyo.

“Mwanafunzi anayehitaji mkopo huu anaweza kuupata moja kwa moja kupitia simu ya mkononi,” alieleza Bw Kimori.

Waziri Mkuu alipohoji jinsi wananchi wasiokuwa na akaunti pamoja na sifa za kukopa wanavyosaidiwa na NMB, Bw Kimori alisema ipo taasisi mahususi ya NMB Foundation kwa ajili ya hilo kupitia mpango wa udhamini wa masomo na malezi unaoitwa Nuru Yangu Scholarship and Mentorship Program.

Kupitia mpango huu, NMB imetenga kiasi cha TZS bilioni 1 kwa ajili ya kufadhili wanafunzi waliofaulu vizuri kidato cha sita wanaotoka kwenye familia zenye uhitaji ili waweze kutimiza ndozo zao za kujiunga na elimu ya juu.

“Hadi sasa, zaidi ya wanafunzi 130 kwenye vyuo mbalimbali wanapata ufadhili kupitia mpango huu na lengo letu ni kuongeza idadi ya wanufaika wakiwemo wale walio katika vyuo vya ufundi,” Bw Kimori alibainisha.

Mchango mwingine wa NMB wa kuimarisha upatikanaji wa elimu nchini ni kupitia uwajibikaji na uwekezaji wake kwa jamii ambapo kila mwaka hutenga asilimia moja ya faida baada ya kodi kusaidia kutatua changamoto za kielimu na kiafya pamoja na mazingira.

“Suala la elimu limekuwa ni kipaumbele kwetu kwa miaka mingi sana. Kwa mfano kwa miaka miwili iliyopita benki yetu imesaidia shule 472 kupata madawati ambayo yamewawezesha wanafunzi takriban 80,000 kusoma huku wameketi.

Aidha, alisema NMB imeshirikiana na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi.

Hatua hii imewezesha kuunganishwa moja kwa moja kwa mifumo ya Benki ya NMB na mfumo wa Bodi ya Mikopo ujulikanao kama Digital Disbursement Solution (DiDis) unaowezesha wanafunzi kupata fedha zao kwa haraka na kwa uhakika na hivyo basi kuongeza ufanisi wa huduma za mikopo, kuongeza usawa na usalama kupitia njia hii ya kidijitali.

“Tutaendelea kuboresha ushirikiano huu ili uwe na tija kubwa ziadi,” aliongeza.

Bw Kimori pia alisema benki hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali, Wizara ya Elimu pamoja na Bodi ya Mikopo kuhakikisha elimu bora inatolewa nchini kwani elimu ndiyo msingi mkubwa wa maendeleo endelevu ya taifa lolote.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt Bill Kiwia, alisema ushirikiano na NMB utasaidia pia kufanikisha ukusanyaji wa takwimu sahihi kuhusu wanufaika wa mikopo na ufadhili wa benki hiyo.

No comments:

Post a Comment