Kitomari Banking & Finance Blog is a premier site for banking, finance, business, economic, investment and stock market news as well as selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the World. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.
Thursday, 29 August 2024
NBC YASISITIZA DHAMIRA YAKE KUCHOCHEA UKUAJI BIASHARA, UCHUMI WA BULUU ZANZIBAR
Zanzibar, 29 Agosti 2024 – Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeelezea dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na wafanyabishara wadogo, wa kati na wakubwa kupitia huduma zake mbalimbali za kibenki ili kuchochea ukuaji wa uchumi na mchango wa wadau hao katika kufanikisha agenda ya Uchumi wa Buluu na uwezeshaji wa maendeleo visiwani Zanzibar.
Dhamira hiyo imesisitizwa na Meneja wa benki ya NBC tawi la Zanzibar, Abdul Karim Mkila wakati akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Theobald Sabi, kwenye hafla fupi ya Uzinduzi wa Jukwaa la Kimataifa la Wakuu wa Mashirika na Kampuni visiwani Zanzibar linalofahamika kama ‘The Tanzanite CEO Roundtable, Zanzibar Chapter’ iliyofanyika visiwani humo jana jioni.
Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mudrik Ramadhan Soraga aliongoza uzinduzi wa jukwaa hilo, hafla iliyohudhuriwa pia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi, Uchumi na Uwekezaji) Zanzibar, Sharif Ali Sharif.
Jukwaa hilo liliwakutanisha pamoja viongozi wa kampuni na mashirika kutoka Tanzania, Kenya, Afrika Kusini, Mauritius na mataifa jirani likiwa na lengo la kuimarisha uchumi wa buluu na kuwawezesha wafanyabiashara wa ndani. Benki ya NBC ilikuwa miongoni mwa wadhamini muhimu wa jukwaa hilo.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Bw. Mkila alibainisha umuhimu, nia na mchango wa benki hiyo katika kushirikiana na wafanyabiashara pamoja na wadau mbalimbali visiwani humo ili kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia huduma zake mbalimbali zilizobuniwa mahususi kwa ajili yao ikiwemo mikopo na huduma za bima.
"Kimsingi ni kwamba NBC tumejizatiti kushirikiana na wadau wote katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Jukumu letu ni kuhakikisha tunawawezesha wafanyabiashara wadogo, wa kati, na wakubwa kwa kuwapatia huduma bora za kibenki, mikopo na bima, ili waweze kufanya biashara zao kwa ufanisi zaidi," alisema Bw. Mkila.
Aidha, aliongeza kuwa benki hiyo itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwezesha maendeleo ya kiuchumi kwa kuleta ushirikishwaji wa kifedha kwa wafanyabiashara wa sekta zote.
Mbali na wakuu wa kampuni na mashirika, jukwaa hilo lililokuwa na kaulimbiu ‘’Kuimarisha Biashara za Ndani na Kujenga Uchumi Imara wa Buluu Zanzibar,” pia liliwakutanisha wadau wengine wa biashara na uchumi wakiwemo wawekezaji. Washiriki walipata wasaa muhimu wa kubadilishana mawazo, uzoefu, na mbinu za kukuza biashara na fursa za uwekezaji visiwani Zanzibar.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri Soraga, alitoa wito kwa washiriki kuendelea kushirikiana kwa ukaribu zaidi ili kukuza uchumi wa visiwa hivyo hususani kupitia katika sekta za utalii, biashara, uvuvi na ujenzi wa makazi.
"Tukio hili ni nafasi adimu kwa wafanyabiashara, wakuu wa taasisi, na wadau mbalimbali kukutana na kujadili kwa kina masuala muhimu kuhusu uwekezaji na ukuaji wa uchumi. Serikali pia tunalitegemea jukwaa hili kama moja ya namna bora zaidi katika kutusaidia kwa kutupatia ushauri kwenye masuala mbalimbali ya kiuchumi ili kuleta maendeleo endelevu na jumuishi," alisema Waziri Soraga.
Kwa upande wake Waziri Sharif, alisisitiza umuhimu wa wakuu wa makampuni kukutana mara kwa mara ili kujadili fursa na changamoto zinazokabili sekta mbalimbali za kiuchumi kwa kuwa mijadala na maoni yao kwa kiasi kikubwa yatasaidia kuimarisha mazingira ya uwekezaji na kukuza uchumi wa Zanzibar hususani kupitia agenda ya uchumi wa buluu.
“Kwa ujumla uzinduzi wa jukwaa hili la The Tanzanite CEO Roundtable, Zanzibar Chapter unatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo huku ukisaidia kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sekta za uwekezaji na biashara, na kuleta mchango mkubwa kwa ustawi wa uchumi wa Zanzibar.’’ Alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment