Foreign Exchange Rates

DStv Advert_090724

DStv Advert_090724

SBT Tanzania Advert_291123

Monday, 13 May 2024

MIAKA 10 YA USHIRIKIANO KWENYE TIBA YA DHARURA KATI YA MFUKO WA ABBOTT NA WIZARA YA AFYA UNAVYOOKOA MAISHA NCHINI TANZANIA

Mkuu wa Idara ya Tiba za Dharura katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo, Dkt. Arafa Kachenje (kulia), akimhudumia Elly Amdason Kimodoa, mmoja wa wagonjwa walionufaika na huduma za dharura. Kushoto ni muuguzi katika hospitali hiyo, Scholastic Kideka Mundu.
Daktari Said Izina (wa kwanza kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na wahudumu wa afya katika zahanati ya kijiji cha Bantu wilayani Mkinga mkoani Tanga wakati wa ziara ya Abbott Fund katika zahanati hiyo kujionea maendeleo ya huduma za Tiba ya Dharura.
Mkurugenzi Mtendaji wa Abbott Fund nchini Tanzania, Prof. Hendry Sawe akielezea mafanikio ndani ya miaka 10 ya mradi wa Tiba za Dharura unaotekelezwa na mfuko huo kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Afya.
  • Tiba za Dharura ni sehemu muhimu ya huduma za matibabu, lakini maeneo mengi ulimwenguni yana upungufu wa miundombinu ya kutolea huduma hii
  • Mfumo bora wa uendeshaji na utoaji huduma za tiba ya dharura unaisaidia Hospitali ya Taifa nchini Tanzania kuendelea kutoa huduma bora kwa wote
Dar es Salaam, Tanzania, 9 Mei 2024 - Miaka 14 tu iliyopita, Tanzania haikuwa na hospitali hata moja yenye kitengo maalumu cha kutoa huduma za tiba ya dharura na ajali, na vifo katika hospitali ya taifa vilikuwa takribani asilimia 14. Wakati mwingine, wagonjwa ambao walihitaji huduma muhimu za kuokoa maisha, walilazimika kusubiri masaa kadhaa kabla ya kuonwa na madaktari bingwa ambao hawakuwa na utaalamu wa kutosha katika kutoa Tiba za Dharura.

Taasisi ya uhisani ya Abbott inayofahamika kama Mfuko wa Abbott (Abbott Fund) ilianza kushirikiana na Serikali ya Tanzania mwaka 2001 kuimarisha mifumo ya huduma za afya nchini kupitia ushirikiano wa umma na binafsi wenye thamani ya dola za kimarekani zaidi ya milioni 160 ambao unajumuisha mipango mipana ya kusaidia watoto na familia kupata elimu na kuboresha maisha ya wananchi nchini kote.

Kupitia ushirikiano na Serikali ambao umedumu kwa zaidi ya muongo mmoja, Mfuko wa Abbott mnamo mwaka 2010, ulisaidia kuanzisha Idara ya Tiba za Dharura (inayofaamika kifupi kama EMD) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, na kuanzishwa kwa mafunzo ya madaktari bingwa wa tiba ya dharura katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili - zote zikiwa za kwanza Afrika Mashariki. Jitihada hizi zilipata matokeo ya haraka, ambapo vifo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili vilipungua kwa takribani asilimia 40 katika kipindi cha miaka miwili ya kwanza, na kundi la kwanza la madaktari bingwa wa mafunzo ya matibabu ya dharura walihitimu mwaka 2013.

Uanzishwaji wa Mfumo wa Tiba za Dharura nchini Tanzania

Ndani ya kipindi cha miaka mitano, Idara ya Tiba za Dharura katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ilifanikiwa kuweka mifumo bora ya uendeshaji na utoaji huduma za tiba ya dharura ambayo mpaka sasa inatumika kama mfano wa utoaji huduma bora za dharura katika sekta ya afya hapa nchini. Mifumo hii ilisaidia idara hii kupunguza utegemezi kutoka kwa wafadhili na kuweza kuhudumia wa Tanzania kwa uendelevu bila kupoteza viwango katika utoaji huduma.

Leo hii, wagonjwa wanaofika Hospitali ya Taifa Muhimbili wanapata huduma bora za kisasa katika idara ambayo inaweza kuhudumia hadi watu 50,000 kila mwaka.

Kupanua Wigo wa Huduma ya Dharura

Kutokana na mafanikio makubwa na uendelevu wa Idara ya Tiba za Dharura Muhimbili, kuanzia mwaka 2017, Mfuko wa Abbott kwa kushirikiana na Serikali, ulianzisha vituo vya Tiba za Dharura katika maeneo 8 zaidi nchini Tanzania, ikiwemo Mbeya, Arusha, Dodoma, Tanga na Pwani.

Mfuko wa Abbott umetoa msaada wa zaidi ya dola za marekani milioni 15 katika kuanzisha na kuendeleza Tiba za Dharura nchini Tanzania, na hivyo kuendelea kuokoa maisha ya watanzania, ambapo zaidi ya watu milioni 1.2 wamepokea huduma za Tiba za Dharura kuanzia mwaka 2010 kupitia vituo vya Tiba za Dharura vinavyoendeshwa kwa ushirikiano na Mfuko wa Abbott. Kwa upande mwingine, programu ya mafunzo kwa watumishi walioko makazini imetoa mafunzo katika fani ya tiba ya dharura na ajali kwa zaidi wahudumu wa afya 6,000.

Serikali ya Tanzania kwa sasa inatekeleza upanuzi wa huduma za Tiba za Dharura ambao ni mradi mkubwa zaidi wa Tiba za Dharura katika nchi za Kusini mwa Afrika, na imeanzisha idara mpya za Tiba za Dharura katika zaidi ya hospitali 100 katika ngazi ya wilaya na mikoa kote nchini.

Ushirikiano huu baina ya serikali na sekta binafsi unapanua wigo wa Tiba za Dharura na kufikia mamilioni ya watu katika maeneo ambayo hapo awali yalikuwa hayana huduma hiyo. Mfuko wa Abbott unasaidia upanuzi huu kwa kutoa ushauri wa kitaalamu, msaada wa kiufundi katika usanifu wa vituo na mifumo, na pia kutoa mafunzo kwa wafanyakazi yanayoendeshwa kwa ushirikiano na Chama cha watoa huduma za Tiba za Dharura Tanzania (kinachofaamika kama EMAT).

Kujenga Uwezo wa Wahudumu wa Tiba za Dharura

Mapinduzi katika Tiba za Dharura yamechagizwa na timu ya madaktari vijana wa Kitanzania ambao walijitolea kujifunza taaluma mpya ya matibabu na kisha kuongoza harakati za kuokoa maisha na kuboresha huduma za afya nchini.

Mwaka 2023, unaadhimisha miaka 10 tangu kundi la kwanza la madaktari bingwa, kuhitimu mafunzo ya Tiba za Dharura nchini Tanzania; Kundi hili la kwanza, lilijumuisha aliye Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Abbott Tanzania, Prof. Hendry Sawe, Mkuu wa Idara ya Tiba za Dharura Muhimbili, Dk. Juma Mfinanga, Dr. Philip Koka, Dr. Faith Ringo, Dr. Sifael Mgalula, Dr. Shaina Yusuf, Dr. Esmail Sangey, na Marehemu Dr. Upendo George, ambao kwa pamoja, waliweza pia kuanzisha Chama cha watoa huduma za Tiba za Dharura Tanzania (EMAT), ambacho kinatoa mafunzo kwa kizazi kijacho cha wataalamu wa Tiba za Dharura ili kukuza Tiba za Dharura kupitia utafiti, utetezi na ushirikiano.

Kupitia mpango wa Mafunzo ya Tiba za Dharura, hadi sasa, madaktari waliobobea katika tiba ya dharura 88 na watoa huduma za afya zaidi ya 6,000 wamehitimu mafunzo ya vitendo wakiwa kazini. Idadi kubwa ya wahitimu hao wanaongoza utoaji wa tiba za dharura katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania.

Wakati juhudi za Abbott zinalenga kupanua tiba za dharura nchini Tanzania, Idara ya Tiba za Dharura Muhimbili, imekua ikitumika kama kama mfano wa tiba za dharura kwa nchi nyingine barani Africa. Mpaka sasa, madaktari, wauguzi na wahudumu wengine wa afya kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ethiopia, Malawi, Uganda, Kenya na Msumbiji wamepatiwa mafunzo kutoka kwenye Idara ya Tiba za Dharura katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Muundo wa mafunzo wa Madaktari bingwa ulitumika kama mfano na Shirikisho la Tiba za Dharura Afrika (inayofahamika kwa kifupi kama AFEM), na kutumika nchini Ethiopia na Haiti. Idara ya Tiba za dharura na mafunzi pia huchangia katika kukuza tafiti na uelewa wa tiba za dharura. Idara hii ni moja ya taasisi nne ambazo zilitekeleza mpango wa majaribio wa Shirika la Afya Duniani (yaani WHO) katika utafiti wa tiba kwa wagonjwa wa ajali, leo hii matokeo yake yanasaidia mipango kama hii katika nchi mbalimbali Duniani.

No comments:

Post a Comment