Kitomari Banking & Finance Blog is a premier site for banking, finance, business, economic, investment and stock market news as well as selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the World. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.
Foreign Exchange Rates
Selcom Pesa Advert_110225
Standard Chartered Advert_300125
DStv Advert_090724
Tuesday, 6 February 2024
AfDB YAAHIDI KUENDELEZA USHIRIKIANO NA TANZANIA
Na Benny Mwaipaja, Dodoma
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeshughulikia Nishati, Dkt. Kevin Kariuki, ambapo ameishukuru Benki hiyo kwa kufadhili miradi 29 ya kitaifa na kikanda, yenye thamani ya zaidi ya dola za kimarekani bilioni 3.84.
Dkt. Nchemba amesema jijini Dodoma kuwa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo ambapo kati ya miradi hiyo, miradi 26 ni ya kitaifa na 3 ni ya kikanda ambayo iko katika sekta za miundombinu ya barabara, nishati, maji na kilimo.
Alisema kuwa zaidi ya asilimia 13.6 ya fedha hizo zimeelezwa katika uzalishaji na usambazaji wa nishati ya umeme kupitia miradi 5 ambapo mitatu kati ya hiyo ni ya Kitaifa na mingine miwili ni ya Kikanda inayolenga kuunganisha umeme katika nchi za Afrika Mashariki.
Dkt. Nchemba, aliitaja miradi hiyo kuwa ni Mradi wa Umeme wa Mto Malagarasi (49.5 MW), Kakono (87.8 MW), Gridi ya kaskazini Magharibi (400 KV), Maporomoko ya Maji Rusumo (80 MW) na utakaounganisha nchi za Burundi, Rwanda na Tanzania pamoja na mradi wa umeme unaoziunganisha Kenya na Tanzania.
Dkt. Nchemba alibainisha kuwa Benki hiyo imekubali kushiriki katika Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) wa Kikanda wenye lengo la kuunganisha huduma za usafiri na usafirishaji abiria na mizigo kati ya Tanzania nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambapo mikataba ya mkopo huo nafuu itasainiwa hivi karibuni.
Aliiomba Benki hiyo kusaidia utekelezaji wa mradi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwa ni hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira.
Katika mazungumzo yao Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayesimamia masuala ya Nishati, Dkt. Kevin Kariuki, aliahidi kuwa Benki yake ipo tayari kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwekeza katika Nishati safi ya kupikia, kuendelea kufadhili miradi ya ujenzi wa miudombinu ya usambazaji umeme, kilimo na maji.
Alisema kuwa Tanzania ni nchi ya mfano kwa kupigania matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuahidi kuwa Benki yake itamuunga mkono ili kufanikisha mradi huo.
Katika ziara hiyo, Makamu wa Rais wa Benki hiyo ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Kevin Kariuki, ambaye ni raia wa Kenya, aliambatana na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nchini Tanzania, Dkt. Patricia Raverley.
Mwisho.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment