Dodoma, Julai 19, 2023: Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa, anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika mbio za NBC Dodoma Marathon 2023 zinazotarajiwa kufanyika siku ya Jumapili tarehe 23 Julai 2023.
Mbio za mwaka huu zinalenga kukusanya jumla ya shilingi milioni 500. Fedha hizo zitatumika kusaidia kupambana na kansa ya shingo ya kizazi pamoja na kutoa ufadhili wa masomo kwa wakunga ikiwa ni sehemu ya kusaidia kuongeza wataalamu ili kupunguza vifo vya uzazi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma kuhusu maandalizi ya mbio hizo zilizojizolea umaarufu mkubwa na ambazo zinafanyika kwa mara ya nne mfululizo mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alisema mkoa umejipanga vyema kuwapokea wakiambiaji na wageni wote wataoshiriki.
“Kwanza kabisa napenda kuishukuru benki ya NBC kwa kuandaa mbio hizi zenye faida kubwa kwetu kama nchi. Pili niwahakikishie washiriki wote kuwa sisi kama mkoa wa Dodoma tumejipanga vyema kuwahudumia na kuwafanya wafurahie ujio wao hapa Dodoma pamoja na ushiriki katika mbio za mwaka huu,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi alisema mbio za mwaka huu pamoja na kukusanya fedha ili kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi zitasaidia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kutoa ufadhili wa elimu kwa wanafunzi wanaosomea taaluma ya ukunga ili kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.
“Kupitia mbio hizi za NBC Dodoma Marathon 2023, tunalenga kuchangia katika kuboresha afya ya uzazi kupitia kusaidia kwenye mapambano vifo vinavyoweza kuepukika na ambavyo vinatokana na uzazi kupitia kusaidia kupata wataalamu zaidi katika eneo hili. Tunaamini kupitia mbio hizi tutaweza kuisaidia jamii yetu kupambana na changamoto hii ambayo inaathiri maendeleo ya jamii na nchi kwa ujumla,” alisema
Aliongeza “Vilevile tunaendelea na msaada wetu katika mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi. Mpaka sasa tumefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi milioni 500 zilizosaidia kufikia upimaji wa saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake zaidi ya 23,500 na matibabu kwa zaidi ya wanawake 1,300. Tunajivunia mafanikio haya” alisema.
Mkurugenzi huyo aliwataka Watanzania wote kujitokeza katika mbio hizo ili kujenga faya zao kupitia zoezi la kukimbia lakini wakati huo huo wakisaidia kupambana na saratani ya shingo ya kizazi pamoja na kusaidia kupunguza vifo vya uzazi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri aliishukuru NBC kwa kuiamini wilaya ya Dodoma na kuamua kufanyia mbio hizo wilayani hamu huku akiwahakikishia kuwa maandalizi yamekamilika kufanya mbio hizo kuwea zenye mafanikio.
No comments:
Post a Comment