Foreign Exchange Rates

DStv Advert_090724

DStv Advert_090724

SBT Tanzania Advert_291123

Wednesday, 19 July 2023

UPUNGUFU WA FEDHA ZA KIGENI USILETE HOFU - GAVANA TUTUBA


Upungufu wa fedha za kigeni nchini haujafikia kiwango cha kutia hofu kama inavyooelezwa na baadhi ya wadau, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, ameeleza. 

Akizungumza mwanzoni wa kikao cha Benki Kuu na wafanyabiashara wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni Julai 17, 2023 jijini Dar es Salaam, Gavana Tutuba ingawa kuna upungufu wa fedha za kigeni katika nchi nyingi duniani kutokana na sababu mbalimbali, hakuna sababu ya Watanzania kuwa na wasiwasi. 


“Benki Kuu imeendelea kuchukua hatua mbalimbali na itaendelea kuchukua hatua mahsusi zenye lengo la kuhakikisha kuwa upungufu huo wa fedha za kigeni, ambao upo dunia nzima, hauathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wetu,” amesema Gavana Tutuba. 

Gavana wa Benki Kuu alieleza baadhi ya sababu za upungufu wa fedha za kigeni dunianim, hasa dola ya Marekani ambayo inashikilia asilimia 83 ya biashara za kimataifa, kuwa ni pamoja na janga la UVIKO-19, vita kati ya Urusi na Ukraine, mabadiliko ya tabianchi na sera za fedha za Marekani.


Sababu hizo zimesababisha kupanda kwa bei za bidhaa na huduma mbalimbali ikiwemo usafirishaji, na hivyo kuongeza mahitaji ya dola; kuvurugika kwa mfumo wa ugavi, wawekezaji wengi kuwekeza dola zao Marekani. 

Amesema Benki Kuu imeendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa upatikanaji wa dola na sarafu nyingine na kigeni, na kuchukua hatua stahiki kuhakikisha kuwa uchumi wa nchi yetu hauathiriwi sana na changamoto hii. 

Napenda kuwajulisha kuwa, licha ya changamoto hii ya kidunia, nchi yetu imeendelea kuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni (kiasi kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kwa miezi isiyopungua minne). Mathalan, tarehe 14 Julai 2023, nchi yetu ilikuwa na akiba ya fedha za kigeni kiasi cha dola za Marekani bilioni 5.55, ambacho kinakidhi uagizaji wa bidhaa na huduma kwa takriban miezi 5. 

“Hata hivyo, mafanikio haya hayatufanyi tubweteke; ndiyo maana tumeitisha mkutano huu leo ili tujadiliane namna bora zaidi ya kuwafikishia wananchi wetu huduma ya kubadilisha fedha za kigeni,” ameeleza Gavana Tutuba katika kikao hicho kilichowakutanisha wadau wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni zaidi ya 70. 

Gavana Tutuba amewataka wenye maduka ya kubadilisha fedha za kigeni kuendelea kudumisha ushirikiano kwa kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo kwa manufaa yetu na taifa letu kwa ujumla. 

“Kwa kufanya hivi, tutakuwa tunamuunga mkono Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika jitihada zake za kuhakikisha kuwa uchumi wa nchi yetu unakua kwa kasi na wananchi wetu walio wengi wananufaika na ukuaji huo wa uchumi,” ameeleza Bw. Tutuba.

Katika mkutano huo Benki Kuu na wenye maduka ya kubadilisha fedha za kigeni wanajadiliana juu ya namna bora zaidi ya kusimamia na kuendesha biashara ya kubadilisha fedha za kigeni kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo mbalimbali iliyotolewa na Benki Kuu. 

Lengo la kufanya hivyo ni kuongeza ufanisi katika biashara na upatikanaji wa huduma hiyo muhimu, hasa katika kipindi hiki ambacho nchi nyingi duniani zimekumbwa na uhaba wa dola ya Marekani.

No comments:

Post a Comment