Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kulia), akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya UK Export Finance Bw. Tim Reid, baada ya kikao chao. |
Na Benny Mwaipaja, Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameishukuru Taasisi ya Uingereza inayohusika na utoaji mikopo ya UK Export Finance (UKEF), kwa kukamilisha mchakato wa utoaji fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi kadhaa ya maendeleo nchini Tanzania ukiwemo mradi wa upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Pemba na ujenzi wa miundombinu ya barabara visiwani humo.
Dkt. Nchemba ametoa pongezi hizo jijini Dodoma, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa UK Export Finance (UKEF), aliyepo nchini kwa ziara ya kikazi.
Alisema kuwa miradi hiyo, si tu kwamba itachokea shughuli za kiuchumi za visiwa hivyo ukiwemo utalii, bali pia itaboresha maisha ya wananchi wa Tanzania kwa ujumla.
Dkt. Nchemba aliiomba taasisi hiyo, kuangalia uwezekano wa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kipande cha tano na sita cha reli ya kisasa kinachoanzia Isaka hadi Mwanza chenye urefu wa kilometa 249 na mradi wa maji wa Bwawa la Farkwa kwa ajili ya kuondoa changamoto ya uhaba wa maji katika Jiji la Dodoma.
Alisema kuwa Mradi wa reli ya kisasa unaombewa ufadhili wa kipande cha Isaka hadi Mwanza ambao taratibu zake za ununuzi zimekamilika na mkandarasi amepatikana pamoja na kipande cha reli cha kuanzia Kaliua hadi Kalemi kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo ambao uko katika hatua za ununuzi, utafungua biashara katika ukanda huo na kuchochea uchumi na maendeleo ya watu.
Dkt. Nchemba aliiomba Taasisi hiyo kuitafutia Tanzania wawekezaji watakao wekeza katika miradi mbalimbali ya uzalishaji ukiwemo mradi wa barabara ya kulipia ya Chalinze hadi Morogoro ambayo baadae imekusudiwa kufika hadi Dodoma.
Alisema kuwa miradi hiyo ni mkakati wa Serikali, ikiongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, wenye lengo la kukuza ajira kwa vijana na kukuza uchumi wa nchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa UK Export Finance (UKEF), Bw. Tim Reid, aliihakikishia Tanzania kupata fedha kwa ajili ya miradi hiyo lakini pia kuendelea kufadhili miradi mingine ya kimkakati itakayowasilishwa na Serikali ikiwemo maji na nishati.
Alisema kuwa Taasisi hiyo imekamilisha mchakato wa upatikanaji wa fedha kwa ajili ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Pemba pamoja na ujenzi wa miundombinu ya barabara Visiwani Zanzibar na kwamba fedha hizo zitatolewa mara tu baada ya kusainiwa kwa makubaliano ya kimkataba.
Uk Exporter Finance ni Wakala wa Serikali ya Uingereza inayojihusisha na kusaidia uagizaji na uingizaji wa bidhaa nchini humo kwa kutoa mikopo ya mitaji na kukatia bima bidhaa hizo lakini pia kuhakikisha kuwa zinakuwa na bei shindani kwenye masoko.
No comments:
Post a Comment