Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimekubaliana kuondoa vikwazo kumi vya kibiashara visivyo vya kiforodha (NTBs), huku vikwazo nane vikiendelea kushughulikiwa, na vikwazo vingine vipya vinne vimewasilishwa ili kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara baina ya nchi hizo.
Vilevile, nchi hizo zimekubaliana kutoza kiwango cha dola 10 za kimarekani kwa kilomita 100 kwa ajili ya matumizi ya barabara (road user charge) kwa magari ya mizigo kutoka nchi moja kwenda nyingine katika Jumuiya hiyo badala ya kila nchi kuwa na viwango vyake vya tozo.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika Mkutano wa 42 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji la Jumuiya ya Afrika Mashariki (SCTIFI) uliofanyika tarehe 03 Juni, 2023 katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo, Jijini Arusha.
Wakizungumza baada ya Mkutano huo, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, wamesema kuwa Baraza hilo la Mawaziri wa Kisekta, limekubaliana kutoza dola 10 za kimarekani kwa kilomita 100 kwa ajili ya matumizi ya barabara kwa malori ya mizigo yanayofanya safari katika nchi wanachama badala ya kila nchi kutoza gharama zake, pamoja na kuimarisha utoaji huduma za forodha katika mpaka wa Kenya na Tanzania, kutapunguza msongamano wa malori na kuchochea ukuaji wa biashara.
Aidha, Baraza hilo la Mawaziri la Kisekta, limekubaliana kuondoa gharama ya viza kwa watu wanaotaka kusafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine kwa shughuli mbalimbali zikiwemo za kibiashara, ili kukuza mahusiano miongoni mwa wakazi wa Jumuiya hiyo pamoja na kuchochea ukuaji wa biashara na uchumi wa nchi husika.
Kuhusu uondoshaji wa mizigo, Mawaziri hao walifahamishwa kuwa mizigo ya Tanzania inayosafirishwa kwenda Kenya itaendelea kuondoshwa kupitia Mfumo wa Himaya Moja ya Forodha ulioanza kutumika kuanzia mwezi Aprili 2023.
Aidha, Mkutano huo wa Baraza la Mawaziri wa kisekta, umeidhinisha Rasimu ya Mwisho ya Viwango vya Afrika Mashariki (FDEAS) ambapo viwango 65 vitaanza kutumika rasmi, umepitisha Andiko la Kisera kwa ajili ya EAC kufanya majadiliano na maeneo mengine ya Kikanda na nchi nyingine, Hadidu za Rejea kwa ajili ya kuandaa Sera ya Maendeleo ya Sekta Binafsi ya EAC pamoja na Hadidu za Rejea kwa ajili ya kuandaa Mkakati wa Mamlaka za Ushindani kwa kipindi cha mwaka 2024 - 2029. Mkutano huo pia umepitisha kutumika kwa Mfumo wa Kieletroniki wa EAC wa utoaji wa taarifa na utatuzi wa vikwazo vya biashara visivyo vya kiforodha (NTBs) ujulikanao kama NTB App.
Pamoja na makubaliano hayo, Mkutano huo ulipokea na kujadili taarifa ya Mashauriano ya awali ya Bajeti ya Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Utekelezaji wa Maamuzi ya Mkutano wa 41 wa Baraza la Mawaziri wa Kisekta wa Biashara, Viwanda Fedha na Uwekezaji (SCTIFI), Mkutano wa Kamati ya Kisekta ya Biashara, Kamati ya Kisekta ya Uwekezaji, Kamati ya Kisekta ya Masuala ya Forodha, Kamati ya Viwango ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Taarifa ya Mamlaka ya Ushindani ya Afrika Mashariki.
Mkutano huo unaojumuisha nchi wanachama wa EAC ambao ni Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudani Kusini na DR – Congo, hufanyika kwa mujibu wa Kalenda ya Mikutano ya EAC ambapo kwa awamu hii Mkutano huo, uliongozwa na Mwenyekiti ambaye ni Waziri wa Biashara, Uchukuzi, Viwanda na Utalii wa Burundi, Mhe Marie Chantal Nijimbere.
Aidha, Ujumbe wa Tanzania umejumuisha Viongozi na Wataalamu kutoka Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Mtendaji Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC) Bw. William Erio, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Dkt. Athuman Ngenya na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) Bw. Charles Itembe pamoja na Maafisa kutoka Wizara na Taasisi hizo.
No comments:
Post a Comment