Dar es Salaam – Aprili 13, 2023: Katika jitihada za kuhakikisha jamii za Watanzania zinaendelea kunufaika na huduma bora za teknolojia na mawasiliano nchini kote, Vodacom Tanzania PLC imezindua kampeni mpya ijulikanayo kama ‘Zaidi ya Mtandao’ na kuwajulisha wateja wake wapya kuwa sasa wanaweza kutuma na kutoa pesa bila ya tozo kwa miamala chini ya shilingi 50,000.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Biashara na Masoko wa Vodacom Tanzania Plc, wakati wa uzinduzi uliofanyika katika soko la Mabibo jijini Dar es Salaam, Bi. Brigita Shirima ameelezea kuwa kampeni hii mpya ni muendelezo wa namna ambavyo kampuni hiyo yenye Mtandao Supa nchini inagusa maisha ya kila siku ya Watanzania kwenye sekta tofauti za kijamii na kiuchumi kupitia huduma na bidhaa bunifu za kidigitali.
Kampeni ya Zaidi ya Mtandao inahamasisha Watanzania kujiunga na mtandao supa ulioenea nchi nzima na wenye kasi ya 5G. Wateja pia watafurahia vifurushi vya bei nafuu na huduma kemkem za M-Pesa.
“Ni furaha kubwa kuwajulisha Watanzania na haswa wateja wapya kuwa sasa hakutokuwa na makato ya tozo pindi watakapotuma na kupokea pesa chini ya shilingi 50,000. Wateja wetu wapya wataanza kunufaika na huduma hii kuanzia leo ambapo tumezindua kampeni yetu mpya inayojulikana kama ‘Zaidi ya Mtandao’ ambayo imekuja na maboresho ya huduma na bidhaa zetu pamoja na ofa mbalimbali. Miongoni mwa faida kwa mteja mpya wa Mtandao Supa wa Vodacom ni kurudishiwa asilimia 15 ya gharama za bando pindi akinunua vifurushi kupitia M-Pesa,” alisema Bi. Shirima.
Aidha, akifafanua zaidi kwanini ni muhimu kwa wateja wa Vodacom kutumia M-Pesa kununua vifurushi, Mkurugenzi huyo alieleza kuwa hii ni katika harakati za kampuni hiyo kuchangia utunzaji wa mazingira ikiwa ni dhumuni walilojiwekea sambamba na lengo namba 13 la maendeleo endelevu (SDGs).
Mkurugenzi huyo wa Biashara na Masoko alifafanua kuwa Vodacom Tanzania inajivunia kuendelea kuboresha mtandao wake ambapo mwezi Septemba mwaka jana walizindua huduma ya 5G yenye ubora, ufanisi, na iliyoenea nchi nzima kwa shughuli binafsi na za kibiashara. Akielezea sababu moja wapo inayoifanya Vodacom kuwa ‘Zaidi ya Mtandao’ ni kwamba mpaka sasa ina mawakala wa mauzo takribani 29,000 walioenea nchini kote kuwahudumia Watanzania huku wateja wake wakinufaika na faida lukuki za M-Pesa ikiwemo huduma za mikopo nafuu na upatikanaji rahisi wa ‘floti’ kuendeshea biashara zao.
Kwa upande wake Mkuu wa Kanda ya Kaskazini wa kampuni hiyo, Bw. George Venanty, ameongezea kuwa uzinduzi wa kampeni mpya ya ‘Zaidi ya Mtandao’ umefanyika kwa pamoja katika kanda nyingine nne tofauti ambazo ni kanda ya ziwa, kanda ya Dar es Salaam, kanda ya kati na nyanda za juu kusini, ambapo shughuli mbalimbali zitaendelea na kuenea kwingineko kwa lengo la kuwafikia Watanzania wote nchini.
“Vodacom inajivunia kuendelea kutoa huduma za teknolojia na mawasiliano zinazokidhi mahitaji ya Watanzania wote nchini. Mimi na timu yangu ya mawakala wa usajili tupo tayari kuipeleka habari hii nzuri kwa wateja kwenye mitaa tofauti ya jiji la Arusha na viunga vyake pamoja na mikoa ya jirani,” alisema Bw. Venanty.
Kampuni hiyo inaamini kwamba washirika na wadau wake waliotapakaa nchini kote wataendelea kuwaunga mkono kupitia ushirikiano walionao kwa miaka mingi katika kuhakikisha Watanzania wote wanafikiwa na huduma bora na nafuu za mawasiliano.
Vodacom imeendelea kuboresha huduma na bidhaa zake kupitia ubunifu wa kidigitali kama vile kupata mikopo ya wateja binafsi kupitia Songesha na M-Pawa, pamoja na VodaBima inayowawezesha kupata bima kwa kuweka pesa kidogo kidogo kupitia M-Pesa kwenye simu zao za mkononi.
Vile vile, kwa upande wa huduma kwa wateja, hizi zimeboreshwa zaidi ili kumuwezesha mteja kujihudumia mwenyewe kupitia My Vodacom App, kupiga simu, jumbe fupi, WhatsApp pamoja na kurasa rasmi za mitandao ya kijamii ya kampuni hiyo.
Hii yote ni katika kuonyesha jinsi ambavyo Vodacom inamthamini mteja wake na hivyo mbali na huduma za mawasiliano, imejikita katika kubadilisha maisha yake kuptia teknolojia na ndio maana tunasema Vodacom ni Zaidi ya Mtandao.
No comments:
Post a Comment