Foreign Exchange Rates

DStv Advert_020324

DStv Advert_020324

SBT Tanzania Advert_291123

Friday 31 March 2023

SHULE 20 TABORA ZAKABIDHIWA VIFAA VYA TEHAMA VYENYE THAMANI YA TSHS 150 MILIONI NA VODACOM TANZANIA FOUNDATION



Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mh. Balozi Dk. Batilda Buriani (kulia) akipokea msaada wa mojawapo ya kompyuta na vifaa vingine vya TEHAMA vyenye thamani ya shilingi milioni 150 kwa shule za sekondari 20 kutoka kwa Meneja Mauzo Mwandamizi wa Vodacom Tanzania Plc Kanda ya Ziwa, Bw. Ahmed Akbarali (katikati) ikiwa ni sehemu ya mradi wa uunganishwaji wa shule za sekondari unaolenga kuziunganisha shule 300 Tanzania, (school connectivity project), kwa kushirikiana na African Child Projects na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF). Akishuhudia makabidhiano hayo yaliyofanyika katika shule ya sekondari Kariakoo mkoani humo, kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora, Bi. Neema Kapesa.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mh. Balozi Dkt. Batilda Buriani (katikati) akishuhudia makabidhiano ya msaada wa mojawapo ya kompyuta na vifaa vingine vya TEHAMA vyenye thamani ya shilingi milioni 150 kwa shule za sekondari 20 kutoka kwa Meneja Mauzo Mwandamizi wa Vodacom Tanzania Plc Kanda ya Ziwa, Bw. Ahmed Akbarali (kushoto) kwenda kwa Mkurugenzi wa Shirika la Youth Relief Foundation, Bw. Joachim William (kulia), ikiwa ni sehemu ya mradi wa uunganishwaji wa shule za sekondari unaolenga kuziunganisha shule 300 Tanzania (school connectivity project), kwa kushirikiana na African Child Projects na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).

Afisa Elimu Taluma Sekondari Mkoa wa Tabora, Bi. Rosemary Massawe (kushoto) akikabidhi mojawapo ya kompyuta kwa mwalimu mkuu wa Shule ya Sekondari Kariakoo, Bw. Leonard Nyasebwa (kulia) huku Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Manispaa ya Tabora, Bi. Neema Kapesa akishuhudia. Vodacom Tanzania Foundation imesaidia vifaa vya TEHAMA vyenye thamani ya shilingi milioni 150 kwa shule za sekondari 20 mkoani humo ikiwa ni sehemu ya mradi wa uunganishwaji wa shule za sekondari unaolenga kuziunganisha shule 300 Tanzania (school connectivity project), kwa kushirikiana na African Child Projects na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kariakoo ya Tabora, wakijisomea kwenye chumba cha kompyuta baada ya kupokea msaada wa vifaa tofauti vya TEHAMA kutoka Vodacom Tanzania Foundation. Msaada huo wenye thamani ya shilingi milioni 150 ulitolewa kwa shule za sekondari 20 mkoani humo ikiwa ni sehemu ya mradi wa uunganishwaji wa shule za sekondari unaolenga kuziunganisha shule 300 Tanzania (school connectivity project), kwa kushirikiana na African Child Projects na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).

Tabora – Machi 30, 2023: Vodacom Tanzania Foundation imekabidhi msaada wa vifaa vya TEHAMA vyenye thamani ya zaidi ya shilingi 150 milioni kwa shule za sekondari 20 mkoani Tabora ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa uunganishwaji wa shule kwa kushirikiana na taasisi ya African Child Projects na Mfuko wa Mawasiliono Sawa kwa Wote (UCSAF) ambao unalenga kuzifikia shule 300 nchini kote.



Akizungumza wakati wa hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika katika Shule ya Sekondari Kariakoo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Buriani alipongeza jitihada za mpango wa uunganishwaji wa shule katika kuboresha mfumo tulionao sasa wa ufundishaji na kujifunzia kuhamia kwenye mfumo wa kidigitali.



“Umefikia wakati wa kutumia ipasavyo maendeleo yaliyoletwa na mtandao wa intaneti kwa ajili ya manufaa ya jamii zetu. Ninaamini kuwa tunaweza kunufaika kwa kiasi kikubwa endapo tukiitumia vvema huduma ya intaneti bora na ya kuaminika ambayo Vodacom Tanzania inatupatia nchi nzima. Kwa ongezeko la ueneaji wa mtandao wa intaneti na umiliki wa vifaa vya kiteknolojia kama tulivyovipokea leo, sekta ya elimu imebadilika ambako tunaona maendeleo kwenye ufundishaji wa walimu na kujisomea kwa wanafunzi hayategemei tena vitabu pekee” alisema Mh. Balozi Dkt. Buriani.



Mkuu huyo wa Mkoa alifafanua kwamba vifaa hivyo vya TEHAMA vimetolewa katika wakati mzuri ambapo serikali kuu inawekeza kwa kiasi kikubwa kwenye ujenzi wa shule na madarasa, hivyo inatia moyo kuona sekta binafsi inasadia kwenye kuboresha elimu ambayo inatolewa nchini.

Mh Balozi Buriani alichukua nafasi hiyo kuwasihi wanufaika wote kutumia vifaa hivyo ipasavyo ili kuwavutia washirika wengine kujitokeza na hivyo kuongeza vifaa vitakavyotosheleza shule za Mkoa wa Tabora. Aliongeza kwamba anategemea kuona mabadiliko katika ufundishaji na ufaulu ukiongezeka Zaidi.

Kwa upande wake Meneja Mauzo Mwandamizi wa Kanda ya Ziwa Bw Ahmed Akbarali akimuwakilisha Mkuu wa Kanda hiyo wa Vodacom Tanzania Plc, amesisitiza kuwa msaada wa vifaa vya TEHAMA ni sehemu ya utekelezaji wa adhma ya kampuni katika kuboresha maisha ya jamii za Watanzania kupitia ubunifu wa huduma na bidhaa za kidigitali kwenye sekta tofauti nchini kote.

“Ni Fahari kwetu kuchangia vifaa vya TEHAMA kwa shule 20 za mkoani Tabora ambavyo vitasaidia kuboresha maeneo ya ufundishaji na kujisomea kwa walimu na wanafunzi. Vifaa tulivyovikabidhi leo ni pamoja na kompyuta, vishkwambi, luninga, na mashine ya kutolea nakala ambavyo vyote ni muhimu katika kufanikisha matumizi ya mfumo wa e-Fahamu ambao unawarahisishia walimu na wanafunzi kufikia maelfu ya vitabu mtandaoni,” alisema Akbarali.

Meneja huyo Mwandamizi wa Kanda aliongeza kuwa katika awamu hii, baadhi ya shule zitaunganishwa na intaneti ya Vodacom Tanzania kwa mwaka mzima bila ya malipo hii itawasaidia kupata maudhui bure kupitia jukwaa linalotoa elimu kidigitali la e-Fahamu na anatumaini kwamba vifaa walivyotoa vitakuwa msaada mkubwa katika kusaidia kuboresha ufanisi sio kwa walimu na wanafunzi pekee bali kwa sekta nzima ya elimu mkoani Tabora.

Tangu kuanza kwa mpango wa uunganishwaji wa shule mwaka 2019, Vodacom Tanzania Foundation imetoa msaada wa vifaa vya TEHAMA vyenye thamani ya zaidi ya shilingi billioni mbili kwa shule za sekondari katika mikoa mbalimbali nchini kwa kushirikiana na wadau wengine. Programu ya e-Fahamu ni muendelezo wa jitihada za kampuni hiyo kuunga mkono juhudi za serikali kwenye sekta mbalimbali za maendeleo kupitia bunifu na suluhisho za kidigitali.

“Mpaka sasa takribani wanafunzi 600,000 wananufaika na tunatarajia idadi hii kuongezeka kufikia utekelezaji wake kwa ukamilifu. Niwaombe walimu, wanafunzi, na shule kuvitumia vifaa wanavyopokea leo ili kuboresha ufaulu na hivyo kunufaika na matumizi mazuri ya mtandao wa intaneti,” alihitimisha Bw.Akbarali.

Jumla ya vifaa 101 vya TEHAMA ikiwemo kompyuta, vishkwambi, luninga, na mashine ya kutolea nakala (photocopy machine) vilitolewa kwa shule 20 za sekondari zikiwemo Bombamzinga, Milambo, Lwanzari, Kariakoo, Kazehilli, Ipuli, Isevya, Fundikira, Kanyenye, Kazima, Nyamwezi, Nkinga, Ziba, Igunga, Chief Ntinginya, Bugwangoso, Bugwandege, Miguwa, Bulunde, na Undomo ambapo mpango wa uunganishwaji wa shule umeshafikia shule 812 nchini kote toka kuanzishwa kwake.

Akizungumza kwa niaba ya wakuu wenzake wa shule ambazo zimenufaika na msaada huo, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kariakoo, Bw. Leonard Nyasebwa alipongeza juhudi za serikali na sekta binafsi kuwafikishia vifaa hivyo. Alishukuru kwa vifaa vya TEHAMA viliyotolewa kwa sababu vitasaidia katika kufundishia na kujifunzia.

“Ni muda muafaka sasa kuanza kuzingatia uwekezaji kwenye miundombinu ya TEHAMA katika shule zote nchini. Kwa sababu ukiwa na miundombinu ya kiteknolojia huduma ya kufundishia na kujisomea mtandaoni itaweza kuwafikia kwa urahisi na haraka walimu na wanafunzi wote ukilinganisha na vitabu ambavyo kujitosheleza itachukua muda mrefu. Uwepo wa mfumo wa e-Fahamu na kukubalika kutumika kwenye shule za sekondari nchini ni dalili nzuri kwamba tupo tayari kubadilika ili kuendana na dunia ya kidigitali,” aliongeza

Programu ya e-Fahamu ilianzishwa na Vodacom Tanzania Foundation mnamo mwaka 2017 kwa lengo la kuwasaidia walimu na wanafunzi kupata vitabu vya ziada na kiada kwa shule za msingi na sekondari ambavyo vinafuata mitaala ya kutoka maktaba ya Taasisi ya Elimu Tanzania na masomo ya kimataifa bure kwa njia ya mtandao. Lengo la jukwaa hilo ni kuunga mkono juhudi za Serikali za kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari nchini.

Kwa kumalizia muwakilishi kutoka Vodacom aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na TAMISEMI kwa ushirikiano mkubwa wanaoendelea kuipatia Vodacom katika shughuli zake za maendeleo kwa jamii katika nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya kilimo na afya.

No comments:

Post a Comment